Mathayo 21
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Yesu Aingia Yerusalemu Kama Mfalme
(Mk 11:1-11; Lk 19:28-38; Yh 12:12-19)
21 Yesu na wafuasi wake walipokaribia Yerusalemu, walisimama Bethfage kwenye kilima kinachoitwa Mlima wa Mizeituni. Wakiwa hapo Yesu aliwatuma wafuasi wake wawili mjini. 2 Aliwaambia, “Nendeni kwenye mji mtakaoweza kuuona huko. Mtakapoingia katika mji huo, mtamwona punda na mwanapunda wake.[a] Wafungueni wote wawili, kisha waleteni kwangu. 3 Mtu yeyote akiwauliza kwa nini mnawachukua punda, mwambieni, ‘Bwana anawahitaji. Atawarudisha mapema.’”
4 Hili lilitimiza maneno yaliyosemwa na nabii:
5 “Waambie watu wa Sayuni,[b]
‘Mfalme wako anakuja sasa.
Ni mnyenyekevu na amempanda punda.
Na amempanda mwana punda dume tena safi.’”(A)
6 Wafuasi walikwenda na kufanya yale walioambiwa na Yesu. 7 Waliwaleta kwake punda jike na mwanapunda. Waliwafunika punda kwa nguo zao na Yesu akaketi juu yao. 8 Akiwa njiani kuelekea Yerusalemu, watu wengi walitandaza mavazi yao barabarani kwa ajili Yake. Wengine walikata matawi ya miti na kuyatandaza barabarani ili kumkaribisha. 9 Wengine walimtangulia Yesu, na wengine walikuwa nyuma yake. Wote walipaza sauti wakisema:
“Msifuni[c] Mwana wa Daudi!
‘Karibu! Mungu ambariki yeye
ajaye katika jina la Bwana!’(B)
Msifuni Mungu wa mbinguni!”
10 Kisha Yesu aliingia Yerusalemu. Watu wote mjini wakataharuki. Wakauliza, “Mtu huyu ni nani?”
11 Kundi la watu waliomfuata Yesu wakajibu, “Huyu ni Yesu. Ni nabii kutoka katika mji wa Nazareti ulio Galilaya.”
Yesu Asafisha Eneo la Hekalu
(Mk 11:15-19; Lk 19:45-48; Yh 2:13-22)
12 Yesu alipoingia katika eneo la Hekalu, aliwatoa nje wote waliokuwa wanauza na kununua vitu humo. Alizipindua meza za watu waliokuwa wanabadilishana pesa. Na alipindua viti vya watu waliokuwa wanauza njiwa. 13 Yesu aliwaambia, “Maandiko yanasema, ‘Hekalu langu litaitwa nyumba ya sala.’(C) Lakini mmelibadilisha na kuwa ‘maficho ya wezi’.(D)”
14 Baadhi ya watu waliokuwa wasiyeona na walemavu wa miguu walimjia Yesu alipokuwa eneo la Hekalu, naye aliwaponya. 15 Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria waliona mambo ya ajabu aliyokuwa anatenda. Na waliona watoto walivyokuwa wanamsifu wakisema, “Sifa kwa Mwana wa Daudi.” Mambo haya yote yaliwakasirisha makuhani na walimu wa sheria.
16 Wakamwuliza Yesu, “Unasikia wanayosema watoto hawa?”
Akajibu, “Ndiyo. Maandiko yanasema,
‘Umewafundisha watoto wadogo na watoto
wanyonyao kusifu.’(E)
Hamjasoma Maandiko haya?”
17 Kisha Yesu akawaacha na akaenda katika mji wa Bethania akalala huko.
Yesu Aulaani Mtini
(Mk 11:12-14,20-24)
18 Mapema asubuhi iliyofuata, Yesu alikuwa anarudi mjini Yerusalemu naye alikuwa na njaa. 19 Aliuona mtini karibu na njia na akaenda kuchuma tini kwenye mti huo. Yalikuwepo maua tu. Hivyo Yesu akauambia mti ule, “Hautazaa matunda tena!” Mtini ukakauka na kufa hapo hapo.
20 Wafuasi wake walipoona hili, walishangaa sana. Wakauliza, “Imekuwaje mtini ukakauka na kufa haraka hivyo?”
21 Yesu akajibu, “Ukweli ni kuwa, mkiwa na imani na msiwe na mashaka, mtaweza kufanya kama nilivyofanya kwa mti huu. Na mtaweza kufanya zaidi ya haya. Mtaweza kuuambia mlima huu, ‘Ng'oka na ujitupe baharini.’ Na ikiwa una imani, litafanyika. 22 Mkiamini, mtapokea kila mnachoomba.”
Viongozi Wawa na Mashaka Kuhusu Mamlaka ya Yesu
(Mk 11:27-33; Lk 20:1-8)
23 Yesu aliingia katika eneo la Hekalu na akaanza kufundisha humo. Viongozi wa makuhani na viongozi wa wazee wakamjia. Wakasema, “Tuambie! Una mamlaka gani ya kufanya mambo haya unayofanya? Na nani amekupa mamlaka hii?”
24 Yesu akajibu, “Nitawauliza swali pia. Mkinijibu, ndipo nitawaambia nina mamlaka gani ya kufanya mambo haya. 25 Niambieni: Yohana alipowabatiza watu, mamlaka yake ilitoka kwa Mungu au kwa wanadamu?”
Makuhani na viongozi wa Kiyahudi wakajadiliana kuhusu swali la Yesu, wakasemezana, “Tukisema, ‘Ubatizo wa Yohana ulitoka kwa Mungu,’ atasema, ‘Sasa kwa nini hamkumwamini Yohana?’ 26 Lakini hatuwezi kusema ubatizo wa Yohana ulitoka kwa watu wengine. Tunawaogopa watu, kwa sababu wote wanaamini kuwa Yohana alikuwa nabii.”
27 Hivyo wakamwambia Yesu, “Hatujui jibu.”
Yesu akasema, “Basi hata mimi siwaambii aliyenipa mamlaka ya kufanya mambo haya.”
Yesu Atumia Simulizi Kuhusu Wana Wawili
28 “Niambieni mnafikiri nini kuhusu hili: Alikuwepo mtu mwenye wana wawili. Alimwendea mwanaye wa kwanza na kumwambia, ‘Mwanangu, nenda ukafanye kazi kwenye shamba la mizabibu leo.’
29 Mwanaye akasema, ‘Siendi.’ Lakini baadaye akabadili uamuzi wake na akaenda.
30 Kisha baba akamwendea mwanaye mwingine na kumwambia, ‘Mwanangu, nenda ukafanye kazi kwenye shamba la mizabibu leo.’ Akajibu, ‘Sawa baba, nitakwenda kufanya kazi.’ Lakini hakwenda.
31 Ni yupi kati ya wana hawa wawili alimtii baba yake?”
Viongozi wa Kiyahudi wakajibu, “Ni mwana wa kwanza.”
Yesu akawaambia, “Ukweli ni huu, ninyi ni wabaya kuliko watoza ushuru na makahaba. Ukweli ni kuwa hao wataingia katika ufalme wa Mungu kabla yenu. 32 Yohana alikuja akiwaonesha njia sahihi ya kuishi, na hamkumwamini. Lakini watoza ushuru na makahaba walimwamini Yohana. Mliona yaliyotokea, lakini hamkubadilika na mlikataa kumwamini.
Yesu Atoa Simulizi Kuhusu Shamba la Mzabibu
(Mk 12:1-12; Lk 20:9-19)
33 Sikilizeni simulizi hii: Alikuwepo mtu aliyemiliki shamba la mizabibu. Alijenga uzio kuzunguka shamba lile la mizabibu na akachimba shimo kwa ajili ya kukamulia zabibu.[d] Kisha akajenga mnara wa lindo. Akalikodisha shamba kwa wakulima kisha akasafiri. 34 Wakati wa kuvuna zabibu ulipofika, akawatuma watumishi wake waende kwa wakulima ili apate gawio lake la zabibu.
35 Lakini wakulima waliwakamata wale watumishi na kumpiga mmoja wao. Wakamwua mwingine na wa tatu wakampiga kwa mawe mpaka akafa. 36 Hivyo mwenye shamba akawatuma baadhi ya watumishi wengine wengi zaidi ya aliowatuma hapo kwanza. Lakini wakulima wakawatendea kama walivyowatendea watumishi wa kwanza. 37 Hivyo mwenye shamba akaamua kumtuma mwanaye kwa wakulima. Alisema, ‘Wakulima watamheshimu mwanangu.’
38 Lakini wakulima walipomwona mwanaye, wakaambizana, ‘Huyu ni mwana wa mwenye shamba. Shamba hili litakuwa lake. Tukimwua, shamba la mizabibu litakuwa letu.’ 39 Hivyo wakulima wakamchukua mwana wa mwenye shamba, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu na kumwua.
40 Hivyo mmiliki wa shamba la mizabibu atawafanya nini wakulima hawa atakaporudi?”
41 Makuhani wa Kiyahudi na viongozi wakasema, “Kwa hakika atawaua watu hao waovu. Kisha atawakodishia wakulima wengine shamba hilo, watakaompa gawio la mazao yake wakati wa mavuno.”
42 Yesu akawaambia, “Hakika mmesoma hili katika Maandiko:
‘Jiwe walilolikataa waashi
limekuwa jiwe kuu la pembeni.
Bwana amefanya hivi,
na ni ajabu kubwa kwetu kuliona.’(F)
43 Hivyo ninawaambia kuwa, ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu na watapewa watu wanaofanya mambo anayoyataka Mungu katika ufalme wake. 44 Kila aangukaye kwenye jiwe hili atavunjika na litamsaga kila linayemwangukia.”[e]
45 Viongozi wa makuhani na Mafarisayo waliposikia simulizi hizi, wakajua kuwa Yesu alikuwa anawasema wao. 46 Walitaka kumkamata Yesu. Lakini waliogopa kwani watu waliamini kuwa Yesu ni nabii.
Footnotes
- 21:2 mwanapunda wake Kifungu katika Agano la Kale ambacho Mathayo ananukuu mstari wa 5 kinasema wazi kwamba punda wa pili ni mwanapunda.
- 21:5 watu wa Sayuni Kwa maana ya kawaida, “binti Sayuni”, ina maana mji wa Yerusalemu. Tazama Sayuni katika Orodha ya Maneno.
- 21:9 Msifuni Yaani, “Hosanna”, ambalo ni neno la Kiebrania lililotumika kumwomba msaada Mungu. Hapa, labda ilikuwa ni kelele ya shangwe iliyotumika kumsifu Mungu au Masihi wake. Pia mwishoni mwa mstari huu na pia katika mstari wa 15.
- 21:33 shimo kwa ajili ya kukamulia zabibu Au “shinikizo”.
- 21:44 Nakala zingine za Kiyunani hazina mstari wa 44.
Copyright © 2017 by Bible League International