Luka 20:9-19
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Yesu Atoa Simulizi Kuhusu Shamba la Mzabibu
(Mt 21:33-46; Mk 12:1-12)
9 Yesu akawaambia watu kisa hiki; “Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu. Kisha akalikodisha kwa wakulima, kisha akasafiri kwa muda mrefu. 10 Wakati wa kuvuna zabibu ulipofika, alimtuma mmoja wa watumishi wake kwa wakulima wale ili wampe sehemu yake ya zabibu. Lakini wakulima wale walimpiga yule mtumishi na wakamfukuza bila kumpa kitu. 11 Hivyo mtu yule akamtuma mtumishi mwingine. Wakulima walimpiga mtumishi huyu pia, wakamwaibisha na kumfukuza bila kumpa kitu. 12 Hivyo mtu yule akamtuma mtumishi wa tatu. Wakulima wakampiga sana mtumishi huyu na wakamtupa nje ya shamba la mizabibu.
13 Mmiliki wa shamba la mizabibu akasema, ‘Nitafanya nini? Nitamtuma mwanangu mpendwa. Yumkini watamheshimu.’ 14 Lakini wakulima walipomwona mwana wa mwenye shamba, wakajadiliana wakisema, ‘Huyu ni mwana wa mmiliki wa shamba. Shamba hili la mizabibu litakuwa lake. Tukimwua, litakuwa letu.’ 15 Hivyo wakulima wakamtupa mwana wa mmiliki wa shamba nje ya shamba la mizabibu na wakamwua.
Je, mmiliki wa shamba la mizabibu atafanya nini? 16 Atakuja na atawaua wale wakulima, kisha atalikodisha shamba kwa wakulima wengine.”
Watu waliposikia mfano huu, wakasema, “Hili lisije kutokea!” 17 Lakini Yesu akawakazia macho na akasema, “Hivyo basi, Maandiko haya yanamaanisha nini:
‘Jiwe lililokataliwa na wajenzi,
limekuwa jiwe kuu la pembeni?’[a]
18 Kila mtu aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjikavunjika na ikiwa jiwe hilo litaangukia, litakusaga!”
19 Walimu wa sheria na wakuu wa makuhani waliposikia kisa hiki, walijua unawahusu wao. Hivyo walitaka kumkamata Yesu wakati huo huo, lakini waliogopa watu wangewadhuru.
Read full chapterFootnotes
- 20:17 Zab 118:22. Yesu, ambaye ndiye “Jiwe” katika Zaburi hii, anajitambulisha mwenyewe kama mwana katika simulizi hii ambapo anauawa na wakulima wale. Tazama Mdo 4:11.
Copyright © 2017 by Bible League International