Add parallel Print Page Options

Yesu na Ndugu Zake

Baada ya hayo, Yesu alitembea kuizunguka miji ya Galilaya. Hakutaka kutembelea Uyahudi, kwa sababu viongozi wa Kiyahudi kule walitaka kumuua. Huu ulikuwa ni wakati wa sherehe za sikukuu ya Wayahudi ya Vibanda. Hivyo ndugu zake wakamwambia, “Unapaswa kuondoka hapa na kwenda kwenye sikukuu Uyahudi. Kisha wafuasi wako kule wataweza kuona ishara unazofanya. Ikiwa unataka kujulikana, basi usiyafiche mambo unayoyafanya. Ikiwa unaweza kufanya mambo ya ajabu hivi, acha ulimwengu wote uone.” Ndugu zake Yesu walisema hivi kwa kuwa hata wao hawakumwamini.

Yesu akawaambia, “Wakati unaonifaa kufanya hivyo haujafika, lakini kwenu ninyi kila wakati unafaa. Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi. Bali ulimwengu unanichukia mimi kwa sababu nawaambia watu ulimwenguni ya kwamba wanafanya maovu. Hivyo ninyi nendeni kwenye sikukuu. Mimi sitaenda sasa, kwa sababu wakati unaonifaa haujafika.” Baada ya Yesu kusema hayo, akabaki Galilaya.

10 Ndugu zake nao wakaondoka kwenda kwenye sikukuu ya Wayahudi ya Vibanda. Baada ya kuondoka kwao Yesu naye akaenda huko, ingawa hakutaka watu wamwone. 11 Baada ya sikukuu ile kupita viongozi wa Kiyahudi wakawa wanamtafuta Yesu. Wakasema, “Yuko wapi huyo Yesu?”

12 Lilikuwepo kundi la watu wengi mahali pale. Wengi kati yao walikuwa wakizungumza kwa siri kuhusu Yesu. Wengine wakasema, “Huyu ni mtu mzuri.” Lakini wengine wakakataa na kusema, “Hapana, mtu huyo huwadanganya watu.” 13 Pamoja na hayo hakuwepo mtu aliyekuwa na busara zaidi kati yao kusema na Yesu kwa uwazi. Kwani waliwaogopa viongozi wa Wayahudi.

Yesu Afundisha Yerusalemu

14 Sherehe ile ilipokaribia kuisha, Yesu akaenda katika maeneo ya Hekalu na kuanza kufundisha. 15 Viongozi wa Kiyahudi waliomsikiliza walishangazwa na kusema, “Mtu huyu amejifunza wapi mambo haya yote? Yeye hakuwahi kupata mafundisho kama yale tuliyonayo.”

16 Yesu akajibu, “Ninayofundisha siyo yangu. Mafundisho yangu yanatoka kwake Yeye aliyenituma. 17 Watu wanaotaka kufanya kwa uhakika kama anavyotaka Mungu watafahamu kuwa mafundisho yangu yanatoka kwa Mungu. Watafahamu kwamba mafundisho haya siyo yangu. 18 Kama ningeyafundisha mawazo yangu, ningekuwa najitafutia heshima yangu mwenyewe. Lakini kama najaribu kumletea heshima Yeye aliyenituma, basi naweza kuaminiwa. Yeyote anayefanya kama hivyo hawezi kusema uongo. 19 Musa aliwapa sheria, sivyo? Lakini hamuitii hiyo sheria. Kama mnaitii, kwa nini basi mnataka kuniua?”

20 Watu wakamjibu Yesu, “Pepo amekuchanganya akili! Sisi hatuna mipango ya kukuua!”

21 Yesu akawambia, “Nilitenda ishara moja siku ya Sabato, na wote mkashangaa. 22 Lakini mnatii sheria aliyowapa Musa kuhusu kutahiriwa; nanyi mnatahiri hata siku ya Sabato! (Lakini hakika, Musa siye aliyewatahiri. Tohara Ilitoka kwa baba zenu walioishi kabla ya Musa.) Ndiyo, siku zote mnatahiri wana wenu hata siku ya Sabato. 23 Hii inaonesha kuwa mtu anaweza kutahiriwa siku ya Sabato ili kuitimiza sheria ya Musa. Sasa kwa nini mnanikasirikia mimi kwa kuuponya mwili wote wa mtu siku ya Sabato? 24 Acheni kuhukumu mambo ya watu kwa jinsi mnavyoyaona. Muwe makini kutoa kuhukumu kwa njia ya haki kabisa.”

Watu Wajiuliza Ikiwa Yesu Ni Masihi

25 Kisha baadhi ya watu waliokuwepo Yerusalemu wakasema, “Huyo ndiye mtu wanayetaka kumuua. 26 Lakini anafundisha mahali ambapo kila mtu anaweza kumwona na kumsikia. Wala hakuna anayejaribu kumzuia kufundisha. Inawezekana viongozi wamekubali kuwa kweli yeye ni Masihi. 27 Lakini Masihi halisi atakapokuja, hakuna atakayejua anakotoka. Nasi tunajua nyumbani kwake mtu huyu ni wapi.”

28 Yesu alikuwa bado anafundisha katika eneo la Hekalu aliposema kwa sauti, “Ni kweli mnanijua mimi na kule ninakotoka? Niko hapa, lakini siyo kwa matakwa yangu. Nilitumwa na Yeye aliye wa kweli. Lakini ninyi hamumjui. 29 Mimi namfahamu kwa sababu ninatoka kwake. Naye Ndiye aliyenituma.”

30 Yesu aliposema hivi, watu wakajaribu kumkamata. Lakini hakuna aliyethubutu hata kumgusa, kwa sababu wakati unaofaa kufanya hivyo ulikuwa bado haujafika. 31 Hata hivyo watu wengi wakamwamini Yesu. Wakasema, “Je, tunafikiri kuna haja ya kuendelea kumngojea Masihi mwingine aje atakayetenda ishara nyingine zaidi ya zile alizotenda mtu huyu?”

Viongozi wa Kiyahudi Wajaribu Kumkamata Yesu

32 Mafarisayo wakasikia yale ambayo watu walikuwa wakiyasema juu ya Yesu. Kwa sababu hiyo viongozi wa makuhani na Mafarisayo wakawatuma walinzi wa Hekalu kwenda kumkamata. 33 Kisha Yesu akasema, “Nitakuwa nanyi kwa muda mfupi. Kisha nitarudi kwake Yeye aliyenituma. 34 Ninyi mtanitafuta, lakini hamtaniona. Nanyi hamwezi kuja kule nitakapokuwa.”

35 Hawa Wayahudi wakaambiana wao kwa wao, “Huyu mtu atakwenda wapi sisi tusikoweza kufika? Je, anaweza kwenda kwenye miji ya Wayunani wanamoishi watu wetu? Je, atawafundisha Wayunani katika miji hiyo? 36 Anasema, ‘Mtanitafuta, lakini hamtaniona.’ Vile vile anasema, ‘Hamwezi kuja kule nitakapokwenda.’ Maana yake ni nini?”

Yesu Azungumza Juu ya Roho Mtakatifu

37 Siku ya mwisho ya kusherehekea sikukuu ikafika. Nayo Ilikuwa siku muhimu zaidi. Katika siku hiyo Yesu alisimama na kusema kwa sauti kubwa, “Yeyote aliye na kiu aje kwangu anywe. 38 Kama mtu ataniamini, mito ya maji yenye uzima itatiririka kutoka ndani ya moyo wake. Ndivyo Maandiko yanavyosema.” 39 Yesu alikuwa anazungumza juu ya Roho Mtakatifu ambaye alikuwa hajatolewa kwa watu bado, kwa sababu Yesu naye alikuwa bado hajatukuzwa. Ingawa baadaye, wale waliomwamini Yesu wangempokea huyo Roho.

Watu Wanabishana Juu ya Yesu

40 Watu waliposikia maneno aliyosema Yesu, baadhi yao wakasema, “Hakika mtu huyu ni nabii.”[a]

41 Wengine wakasema, “Huyu ni Masihi.”

Na wengine wakasema, “Masihi hawezi kutoka Galilaya. 42 Maandiko yanasema kwamba Masihi atatoka katika ukoo wa Daudi. Na wanasema kwamba atatoka Bethlehemu, mji alimoishi Daudi.” 43 Kwa jinsi hiyo watu hawakukubaliana wao kwa wao kuhusu Yesu. 44 Baadhi yao wakataka kumkamata. Lakini hakuna aliyejaribu kufanya hivyo.

Baadhi ya Viongozi wa Kiyahudi Wakataa Kuamini

45 Walinzi wa Hekalu wakarudi kwa viongozi wa makuhani na Mafarisayo. Makuhani na Mafarisayo wakawauliza, “Kwa nini hamjamleta Yesu?”

46 Walinzi wa Hekalu wakajibu, “Hatujawahi kumsikia mtu akisema mambo ya ajabu kiasi hicho!”

47 Mafarisayo wakajibu, “Kwa hiyo Yesu amewadanganya hata ninyi? 48 Hamuoni kuwa hakuna kiongozi yeyote wala sisi Mafarisayo anayemwamini? 49 Lakini watu hao walio nje wasiojua sheria wamo katika laana ya Mungu.”

50 Lakini Nikodemu alikuwa katika kundi lile. Naye ndiye yule aliyekwenda kumwona Yesu pale mwanzo.[b] Naye akasema, 51 “Sheria yetu haitaturuhusu kumhukumu mtu na kumtia hatiani kabla ya kumsikiliza kwanza na kuyaona aliyotenda?”

52 Viongozi wa Kiyahudi wakajibu, “Wewe nawe utakuwa umetoka Galilaya. Jifunze Maandiko. Hutapata lolote kuhusu nabii[c] anayetoka Galilaya.”

Mwanamke Afumaniwa Akizini

53 Kisha wote wakaondoka na kwenda nyumbani.

Footnotes

  1. 7:40 nabii Huenda walikuwa na maana nabii ambaye Mungu, alimwambia Musa ya kwamba atamtuma. Tazama Kum 18:15-19.
  2. 7:50 Naye ndiye … mwanzo Hadithi juu ya Nikodemo kwenda na kuongea na Yesu katika Yh 3:1-21.
  3. 7:52 kuhusu nabii Nakala mbili za kale za Kiyunani zina “Nabii”, ambayo ina maana “nabii kama vile Musa” anayetajwa katika Kum 18:15. Katika Mdo 3:22 na 7:37 hii inaeleweka kuwa ni Masihi kama katika mstari wa 40 hapo juu.