Yohana 13
Neno: Bibilia Takatifu
Yesu Awaosha Miguu Wanafunzi Wake
13 Ilikuwa siku moja kabla ya sikukuu ya Pasaka. Yesu alijua ya kuwa wakati wake wa kuondoka duniani na kurudi kwa Baba yake umekaribia. Alikuwa amewapenda sana wafuasi wake hapa duniani, akawapenda hadi mwisho. 2 Na wakati alipokuwa akila chakula cha jioni pamoja na wanafunzi wake, shetani alikuwa amekwisha kumpa Yuda Iskariote, mwana wa Simoni, wazo la kumsaliti Yesu. 3 Yesu akijua ya kwamba Baba yake alikwisha mpa mamlaka juu ya vitu vyote; na kwamba yeye alitoka kwa Mungu na alikuwa anarudi kwa Mungu, 4 alitoka mezani akaweka vazi lake kando, akajifunga taulo kiunoni. 5 Kisha akamimina maji katika chombo akaanza kuwaosha wanafunzi wake miguu na kuikausha kwa ile taulo aliyojifunga kiu noni. 6 Alipomfikia Simoni Petro, Petro akamwambia, “Bwana, wewe unaniosha miguu?” 7 Yesu akamjibu, “Hivi sasa huelewi ninalofa nya lakini baadaye utaelewa.” 8 Petro akamjibu, “La, hutaosha miguu yangu kamwe!” Yesu akamwambia, “Kama sitaosha miguu yako, huwezi kuwa mfuasi wangu.” 9 Ndipo Petro akasema, “Kama ni hivyo Bwana, nioshe miguu yangu pamoja na mikono yangu na kichwa changu pia!” 10 Yesu akamwambia, “Mtu aliyekwishaoga ni safi mwili mzima naye hahitaji tena kunawa ila kuosha miguu tu. Ninyi nyote ni safi, isipokuwa mmoja.” 11 Yesu alifahamu ni nani angemsaliti, ndio sababu akasema, “Ninyi nyote ni safi, isipo kuwa mmoja.”
12 Alipomaliza kuwaosha miguu alivaa tena vazi lake, akarudi alipokuwa amekaa, ndipo akawaambia, “Je, mnaelewa maana ya jambo nililowafanyia? 13 Ninyi mnaniita mimi, Mwalimu na Bwana, na hii ni sawa, kwani ni kweli. 14 Kwa hiyo ikiwa mimi niliye Bwana wenu na Mwalimu wenu nimewaosha miguu, ninyi pia hamna budi kuoshana miguu. 15 Mimi nimewaonyesha mfano, ili mtendeane kama nilivyowafanyia. 16 Ninawaambia hakika, mtumishi hawezi kuwa mkuu kuliko bwana wake; wala anayetumwa hawezi kuwa mkuu kuliko aliyemtuma. 17 Kwa kuwa sasa mnafahamu mambo haya, mtabarikiwa na Mungu ikiwa mtayafanya. 18 Siwazungumzii ninyi nyote. Ninawa fahamu wote niliowachagua. Maandiko yaliyotamka, ‘Yeye aliyekula chakula pamoja nami amekuwa msaliti wangu,’ hayana budi kutimia. 19 Ninawaambia mambo haya kabla hayajatokea ili yatakapotokea mpate kuamini ya kuwa mimi ndiye Kristo. 20 Nawahakikishia kuwa mtu anayemkubali na kumpokea ye yote ninayemtuma, ananipokea mimi. Na mtu anayenikubali na kunipokea, anampokea Baba yangu ambaye amenituma.”
Yesu Anatabiri Kuwa Yuda Atamsaliti
21 Baada ya haya Yesu alifadhaika sana moyoni, akasema, “Ninawaambia wazi, mmoja wenu atanisaliti.” 22 Wanafunzi wake wakatazamana kwa wasiwasi, kwa kuwa hawakujua anamsema nani. 23 Mmoja wa wanafunzi ambaye Yesu alimpenda sana alikuwa amekaa karibu sana na Yesu. 24 Kwa hiyo Simoni Petro akamwashiria yule mwanafunzi akamwambia, “Tuambie, ni nani anayemsema.” 25 Yule mwanafunzi akimwegemea Yesu akamwambia, “Tafadhali Bwana tuambie, ni nani unayemzungumzia?” 26 Yesu akajibu, “Ni yule nitakayempa hiki kipande cha mkate baada ya kukichovya.” Kwa hiyo baada ya kuchovya ule mkate akampa Yuda, mwana wa Simoni Iskariote. 27 Mara tu baada ya kukipokea kile kipande cha mkate, shetani akamwingia moyoni. Yesu akamwambia Yuda, “Jambo unalok wenda kufanya, kalifanye haraka.’ ’ 28 Hakuna hata mmoja wa wale wengine waliokuwepo pale mezani aliyeelewa maana ya maneno aliy otamka Yesu. 29 Baadhi yao walidhani kwamba alikuwa anamwagiza akanunue vitu watakavyohitaji kwa ajili ya sikukuu au awape mas kini cho chote, kwa kuwa yeye alikuwa mtunza fedha. 30 Kwa hiyo mara baada ya kupokea ule mkate, Yuda alienda zake nje. Wakati huo giza lilikwisha ingia.
Yesu Anatabiri Kuwa Petro Atamkana
31 Yuda alipokwisha ondoka, Yesu akawaambia, “Wakati ume karibia ambapo watu wataona utukufu wangu mimi Mwana wa Adamu na kwa njia hii watu watauona utukufu wa Mungu. 32 Na ikiwa Mungu atatukuzwa, yeye atanipa mimi utukufu wake, na atafanya hivyo mara. 33 Wapendwa wangu, muda wangu wa kuwa pamoja nanyi umekar ibia kwisha. Mtanitafuta; na kama nilivyowaambia Wayahudi, nina waambia na ninyi: ‘ninapokwenda hamwezi kunifuata’. 34 Nina waachia amri mpya: pendaneni ninyi kwa ninyi. Kama mimi nilivy owapenda, na ninyi mpendane vivyo hivyo. 35 Kama mkipendana hivyo, watu wote watafahamu ya kuwa ninyi ni wanafunzi wangu.”
36 Simoni Petro akamwuliza, “Bwana, kwani unakwenda wapi?” Yesu akamjibu, “Ninapokwenda hamwezi kunifuata sasa, lakini mtanifuata baadaye.” 37 Petro akamwuliza tena, “Bwana, kwa nini siwezi kukufuata sasa? Mimi niko tayari kufa kwa ajili yako.” 38 Yesu akamjibu, “Je, ni kweli uko tayari kutoa maisha yako kwa ajili yangu? Ninakwambia hakika ya kuwa, kabla jogoo hajawika, utakanusha mara tatu kwamba hunijui.”
Copyright © 1989 by Biblica