Add parallel Print Page Options

Je, Wayahudi wana upendeleo wowote kuliko wengine? Je, tohara yao inawasaidia lolote jema? Ndiyo, Wayahudi wana upendeleo mwingi. Lililo muhimu zaidi ni kuwa: Mungu aliwaamini akawapa kazi ya kuzitangaza ahadi zake kwa watu wote. Ni kweli kuwa baadhi ya Wayahudi hawakuwa waaminifu kufanya yale Mungu aliyotaka. Lakini je, hilo laweza kumzuia Mungu kutenda kwa uaminifu yale aliyoahidi? Hapana! Hata ikiwa wengine wote watashindwa kutimiza ahadi zao, daima, Mungu atatekeleza aliyosema. Kama Maandiko yanavyosema kuhusu Mungu,

“Utathibitika kuwa mwenye haki kwa maneno yako,
    na utashinda utakaposhitakiwa na watu.”(A)

Lakini hivi ndivyo wengine hufikiri: Tunapotenda mabaya, inaonesha wazi kuwa Mungu ni wa haki. Je, tunaweza kusema kwamba Mungu hatutendei haki anapotuadhibu? Hapana. Ikiwa Mungu si wa haki atawezaje kuuhukumu ulimwengu?

Ninaposema uongo, inamletea Mungu utukufu, kwa sababu uongo wangu hurahisisha ionekane kuwa yeye ni wa kweli. Hivyo kwa nini nihukumiwe kama mtenda dhambi? Na kwa nini tusiseme, “Tufanye maovu ili jambo jema litokee humo.” Baadhi ya watu wanadai kuwa hivyo ndivyo tunavyofundisha! Wahukumiwe kwa kusema hivyo.

Je, sisi Wayahudi ni bora kuliko wengine? Hapana, nimekwishaonyesha kuwa watu wote, wawe Wayahudi au wasio Wayahudi, wako chini ya nguvu ya dhambi.

Watu Wote Wana Hatia

10 Kama Maandiko yanavyosema,

“Hakuna atendaye haki,
    hakuna hata mmoja.
11 Hakuna hata mmoja anayeelewa,
    hakuna anayetaka kumfuata Mungu.
12 Wote wamegeuka na kumwacha,
    na hawana manufaa kwa yeyote.
Hakuna atendaye mema,
    hakuna hata mmoja.”(B)
13 “Maneno yao ni ya hatari kama kaburi lililo wazi.
    Wanatumia ndimi zao kwa kusema uongo.”(C)
“Maneno yao ni kama sumu ya nyoka.”(D)
14     “Midomo yao imejaa maneno ya laana na hasira.”(E)
15 “Nyakati zote wako tayari kuua mtu.
16     Kila wanakokwenda wanasababisha matatizo na uharibifu.
17 Hawajui jinsi ya kuishi kwa amani.”(F)
18     “Hawamheshimu wala kumcha Mungu.”(G)

19 Tunajua ya kwamba, kile ambacho sheria inasema ni kwa ajili ya wale waliopewa sheria. Hii inamaanisha kuwa watu wote, Wayahudi na wasio Wayahudi, hawana udhuru kwa matendo yao. Hivyo ulimwengu wote unasimama mbele za Mungu na lazima ujibu kwake. 20 Kwa sababu kufuata sheria hakumfanyi mtu akahesabiwa haki mbele za Mungu.[a] Sheria inatuonyesha dhambi zetu tu.

Mungu Anavyowafanya Watu Kuwa Wenye Haki

21 Lakini sasa Mungu ametuonesha jinsi alivyo mwema na mwaminifu. Alivyofanya haihusiani na sheria ingawa sheria na manabii walisema kuwa haya yangetokea. 22 Uaminifu wa wema wa Mungu umedhihirishwa kwetu kupitia imani katika[b] Yesu Kristo. Hufanya hivi kwa wote wanaomwamini Kristo. Kwa sababu kwa Mungu watu wote ni sawa. 23 Ndiyo, watu wote wametenda dhambi na wameshindwa kufikia kiwango cha utukufu wa Mungu kilichokusudiwa kwao. 24 Mungu ameamuru sisi sote tufunguliwe kutoka dhambini. Zawadi hii ya neema yake imekuja kwetu kupitia kile ambacho Kristo Yesu alikifanya ili tuwe huru. 25-26 Mungu alimtoa Yesu kama njia ya kusamehe dhambi za watu kupitia imani katika yeye. Mungu anasamehe watu kwa sababu sadaka ya damu ya Yesu iliwaweka huru na dhambi zao. Mungu alimtoa Yesu kuonesha kuwa hutenda haki na bila upendeleo. Alikuwa sahihi huko nyuma alipovumilia na hakuwaadhibu watu kwa sababu ya dhambi zao. Na katika wakati wetu bado anatenda haki. Mungu alifanya hili ili awahukumu watu pasipo kuwa na upendeleo na kumwesabia haki mtu yeyote aliye na imani katika Yesu.

27 Hivyo, sisi Wayahudi tuna nini cha kujivunia? Hatuna kitu. Mungu amefunga mlango kuzuia nje kiburi cha Kiyahudi. Sheria gani husema hivyo? Sheria inayohimiza matendo? Hapana, ni sheria inayosisitiza imani. 28 Ninamaanisha kuwa watu hufanyika wenye haki na kukubaliwa na Mungu kwa njia ya imani,[c] siyo kwa sababu ya yale wanayotenda ili kuifuata sheria. Hili ndilo tunaloamini. 29 Je, mnadhani kuwa Mungu ni Mungu wa Wayahudi tu? Je, yeye si Mungu wa watu wengine pia? Ndiyo, yeye ni Mungu wa wasio Wayahudi pia. 30 Kuna Mungu mmoja tu. Atawahesabia haki Wayahudi[d] kwa imani yao, na atawahesabia haki wasio Wayahudi[e] kwa imani yao. 31 Je, mnadhani kuwa tunaondoa sheria na kuweka imani hii? Hapana! Kwa kuifuata njia ya imani tunafanya kilichokusudiwa na sheria.

Footnotes

  1. 3:20 Tazama Zab 143:2.
  2. 3:22 imani katika Au “uaminifu wa”.
  3. 3:28 imani Au “uaminifu” [wa Yesu], kama katika mstari wa 25-26. Pia katika mstari wa 30.
  4. 3:30 Wayahudi Kwa maana ya kawaida, “tohara”.
  5. 3:30 wasio Wayahudi Kwa maana ya kawaida, “wasiotahiriwa”.