Warumi 15
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
15 Baadhi yetu hatuna matatizo na mambo haya. Hivyo tunapaswa kuwa wastahimilivu kwa wale wasio imara na wenye mashaka. Hatupaswi kufanya yanayotupendeza sisi 2 bali tufanye yale yanayowapendeza wao na kwa faida yao. Tufanye chochote kinachoweza kumsaidia kila mtu kujengeka katika imani. 3 Hata Kristo hakuishi ili kijaribu kujifurahisha yeye mwenyewe. Kama Maandiko yanavyosema, “Matusi ambayo watu waliyatoa dhidi yako pia yalinifanya niteseke.”(A) 4 Chochote kilichoandikwa zamani kiliandikwa ili kitufundishe sisi. Maandiko haya yaliandikwa ili yatupe matumaini yanayokuja kwa njia ya subira na kutia moyo kunakoletwa nayo. 5 Subira na kuhimiza kote hutoka kwa Mungu. Na ninawaombea ili Mungu awasaidie muwe na nia ile ile ninyi kwa ninyi, kama ilivyo nia ya Kristo Yesu. 6 Kisha ninyi nyote, kwa sauti moja, mtamtukuza Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. 7 Kristo aliwakaribisha ninyi, hivyo nanyi mkaribishane ninyi kwa ninyi. Hili litaleta heshima[a] kwa Mungu. 8 Ndiyo, haya ndiyo maneno yangu kwenu kwamba Kristo alifanyika mtumishi wa Wayahudi ili kuonesha kuwa Mungu amefanya yale aliyowaahidi baba zao wakuu. 9 Na pia alifanya hivi ili wale wasio Wayahudi waweze kumsifu Mungu kwa rehema anazowapa. Maandiko yanasema,
“Hivyo nitakushukuru wewe katikati ya watu wa mataifa mengine;
Nitaliimbia sifa jina lako.”(B)
10 Na Maandiko yanasema,
“Ninyi watu wa mataifa mengine furahini pamoja na watu wa Mungu.”(C)
11 Pia Maandiko yanasema,
“Msifuni Bwana ninyi watu wote wa mataifa mengine;
watu wote na wamsifu Bwana.”(D)
12 Na Isaya anasema,
“Mtu mmoja atakuja kutoka katika ukoo wa Yese.[b]
Atainuka na kutawala juu ya mataifa,
na wataweka matumaini yao kwake.”(E)
13 Naomba kwamba Mungu aletaye matumaini awajaze furaha na amani kadri mnavyomwamini yeye. Na hii isababishe tumaini lenu liongezeke hadi lifurike kabisa ndani yenu kwa nguvu za Roho Mtakatifu.
Paulo Azungumzia Kazi Yake
14 Kaka na dada zangu, najua pasipo mashaka kuwa mmejaa wema na mnayo maarifa yote mnayohitaji. Hivyo kwa hakika mnaweza kushauriana ninyi kwa ninyi. 15 Lakini nimewaandikia ninyi kwa ujasiri wote kuhusu mambo fulani niliyotaka mkumbuke. Nilifanya hivi kwa sababu Mungu alinipa karama hii maalumu: 16 kuwa mtumishi wa Kristo Yesu kwa ajili ya wasio Wayahudi. Natumika kama kuhani ambaye kazi yake ni kuhubiri Habari Njema kutoka kwa Mungu. Alinipa mimi jukumu hili ili ninyi msio Wayahudi mweze kuwa sadaka atakayoikubali, sadaka iliyotakaswa na Roho Mtakatifu.
17 Na hii ndiyo sababu najisikia vizuri kuhusu yale yote yaliyofanyika kwa ajili ya Mungu kwa kuwa mimi ni mali ya Kristo Yesu. 18 Sitazungumzia chochote nilichofanya mwenyewe. Nitazungumza tu kuhusu yale Kristo aliyofanya akinitumia mimi katika kuwaongoza wale wasiokuwa Wayahudi katika kutii. Ni yeye aliyetenda kazi katika yale niliyosema na kufanya. 19 Alitenda kazi kwa ishara za miujiza kwa nguvu ya Roho wa Mungu. Matokeo yake ni kuwa nimewahubiri watu Habari Njema kuhusu Kristo kuanzia Yerusalemu na kuzunguka kote mpaka Iliriko. Na hivyo nimemaliza sehemu hiyo ya wajibu wangu. 20 Imekuwa shabaha yangu daima kuzihubiri Habari Njema katika sehemu ambako watu hawajawahi kusikia juu ya Kristo. Nafanya hivi kwa sababu sitaki kujenga katika kazi ambayo tayari mtu mwingine amekwisha kuianza. 21 Kama Maandiko yanavyosema,
“Wale ambao hawakuambiwa kuhusu yeye wataona,
na wale ambao hawajasikia juu yake wataelewa.”(F)
Mpango wa Paulo Kwenda Rumi
22 Kazi hiyo imenifanya niwe na shughuli nyingi sana na mara nyingi imenizuia kuja kuwaona.
23 Kwa miaka mingi nimetamani kuwatembelea, na sasa nimekamilisha kazi yangu katika maeneo haya. 24 Hivyo nitawatembelea nitakapoenda Hispania. Ndiyo, napanga kusafiri kwenda Hispania na natumaini kuwatembelea nikiwa njiani. Nitakaa kwa muda na kufurahi pamoja nanyi. Kisha natumaini mtanisaidia kuendelea na safari yangu.
25 Sasa ninakwenda Yerusalemu kuwasaidia watu wa Mungu huko. 26 Baadhi yao ni maskini, na waamini kule Makedonia na Akaya walitaka kuwasaidia. Hivyo walikusanya kiasi cha fedha ili wawatumie. 27 Walifurahia kufanya hivi. Na ilikuwa kama kulipa kitu fulani walichokuwa wakidaiwa, kwa sababu kama watu wasiokuwa Wayahudi walikuwa wamebarikiwa kiroho na Wayahudi. Hivyo nao wanapaswa kutumia baraka za vitu walivyonavyo kwa ajili ya kuwasaidia Wayahudi. 28 Naelekea Yerusalemu kuhakikisha kuwa maskini wanapokea fedha hizi zilizotolewa kwa ajili yao.
Nitakapokuwa nimekamilisha hilo, nitaondoka kuelekea Hispania na nikiwa njiani nitasimama ili niwaone. 29 Na ninajua kwamba nitakapowatembelea, nitakuja na baraka zote anazotoa Kristo.
30 Kaka na dada zangu, nawaomba mnisaidie katika kazi hii kwa kuniombea kwa Mungu. Fanyeni hivi kwa sababu ya Bwana wetu Yesu Kristo na pendo ambalo Roho anatupa. 31 Niombeeni ili niokolewe kutokana na wale walioko Yudea wanaokataa kuupokea ujumbe wetu. Pia ombeni kwamba msaada huu ninaoupeleka Yerusalemu utakubalika kwa watu wa Mungu huko. 32 Kisha, nitakuwa na furaha wakati nitakapokuja kuwaona, Mungu akipenda. Na ndipo tutaweza kufurahia muda wa kujengana sisi kwa sisi. 33 Mungu anayetoa amani awe pamoja nanyi nyote. Amina.
Copyright © 2017 by Bible League International