Warumi 11
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Mungu Hajawakataa Watu wake
11 Hivyo ninauliza, “Je, Mungu aliwakataa watu wake?” Hapana! Mimi mwenyewe ni Mwisraeli, wa ukoo wa Ibrahimu, katika kabila la Benjamini. 2 Mungu aliwachagua Waisraeli wawe watu wake kabla hawajazaliwa. Na hajawakataa. Hakika mnajua Maandiko yanavyosema kuhusu Eliya anapomwomba Mungu dhidi ya watu wa Israeli. Anasema, 3 “Bwana, wamewaua manabii wako na kuharibu madhabahu zako. Mimi ndiye nabii pekee niliyebaki hai, na sasa wanajaribu kuniua mimi pia.”(A) 4 Lakini ni jibu gani Mungu alilompa Eliya? Mungu alisema, “Nimejihifadhia watu elfu saba wasiomwabudu Baali.”(B)
5 Ndivyo ilivyo sasa. Mungu amewachagua watu wachache kwa neema yake. 6 Na kama aliwachagua kwa neema yake, hivyo si kwa sababu ya matendo yao yaliyowafanya wawe watu wake. Kama wangefanywa kuwa watu wake kutokana na matendo yao, zawadi yake ya neema isingekuwa zawadi halisi.
7 Hivyo hivi ndivyo ilivyotokea: Watu wa Israeli wanazitaka sana baraka za Mungu, lakini si wote waliozipata. Watu aliowachagua walipata baraka zake, lakini wengine wakawa wagumu na wakakataa kumsikiliza. 8 Kama Maandiko yanavyosema,
“Mungu aliwafanya watu walale usingizi.”(C)
“Mungu aliyafumba macho yao ili wasione,
na aliyaziba masikio yao ili wasisikie.
Hili linaendelea hata sasa.”(D)
9 Na Daudi anasema,
“Watu hawa na wakamatwe na kunaswa
katika tafrija wanazofurahia.
Nyakati hizo nzuri ziwasababishe waanguke
ili wapate adhabu wanayoistahili.
10 Yapofushe macho yao ili wasiweze kuona.
Ipindishe migongo yao kwa mzigo wa matatizo.”(E)
11 Hivyo nauliza: Pale watu wa Mungu walipojikwaa na kuanguka, Je, hawakuweza kuinuka tena? Hakika hapana! Lakini kujikwaa kwao katika mwendo kulileta wokovu kwa wale wasio Wayahudi. Kusudi la hili lilikuwa kuwafanya Wayahudi wapate wivu. 12 Kosa lao na hasara yao vilileta baraka za utajiri kwa ulimwengu kwa wasio Wayahudi. Hivyo fikirini ni kwa kiasi gani baraka hizi zitakuwa kubwa kwa ulimwengu pale idadi ya kutosha ya Wayahudi watakapokuwa watu wa aina ile anayoitaka Mungu.
13 Nasema na ninyi watu msio Wayahudi. Kwa vile mimi ndiye ambaye Mungu ameniteua niwe mtume kwa wale wasio Wayahudi, nitafanya kwa bidii yote kuiheshimu huduma hii. 14 Natarajia kuwafanya watu wangu wawe na wivu. Kwa njia hiyo, labda naweza kuwasaidia baadhi yao waweze kuokolewa. 15 Mungu aliwaacha kwa muda. Hilo lilipotokea, akawa rafiki wa watu wengine ulimwenguni. Hivyo anapowakubali Wayahudi, ni sawa na kuwafufua watu baada ya kifo. 16 Kama sehemu ya kwanza ya mkate inatolewa kwa Mungu, basi mkate mzima unakuwa umetakaswa. Kama mizizi ya mti ni mitakatifu, matawi ya mti huo pia ni matakatifu.
17 Ni kama vile baadhi ya matawi ya mzeituni yamevunjwa, na tawi la mzeituni mwitu limeunganishwa katika ule mti wa kwanza. Ikiwa wewe si Myahudi, uko sawa na tawi la mzeituni mwitu, na sasa unashiriki nguvu na uhai wa mti wa kwanza. 18 Lakini msienende kama mlio bora kuliko matawi yale yaliyovunjwa. Hamna sababu ya kujivuna, kwa sababu hamleti uhai katika mzizi. Mzizi ndiyo huleta uhai kwenu. 19 Mnaweza kusema, “Matawi yalivunjwa ili niweze kuunganishwa katika mti wake.” 20 Hiyo ni kweli. Lakini matawi hayo yalivunjwa kwa sababu hayakuamini. Na mnaendelea kuwa sehemu ya mti kwa sababu tu mnaamini. Msijivune, bali muwe na hofu. 21 Ikiwa Mungu hakuyaacha matawi ya asili ya mti huo yawepo, hataweza kuwaacha ninyi muwepo mtakapoacha kuamini.
22 Hivyo mnaona kwamba Mungu yu mwema, lakini anaweza pia kuwa mkali. Huwaadhibu wale wanaoacha kumfuata. Lakini ni mwema kwenu ikiwa mtaendelea kumwamini katika wema wake. Kama hamtaendelea kumtegemea yeye, mtakatwa kutoka katika mti. 23 Na kama Wayahudi watamwamini Mungu tena, yeye atawapokea tena. Ana uwezo wa kuwarudisha pale walipokuwa. 24 Kwa asili, tawi la mzabibu mwitu haliwezi kuwa sehemu ya mti mzuri. Lakini ninyi msio Wayahudi ni kama tawi lililovunjwa kutoka katika mzeituni pori. Na mliunganishwa na mti wa mzeituni ulio mzuri. Lakini Wayahudi ni kama matawi yaliyostawi kutokana na mti mzuri. Hivyo kwa hakika yanaweza kuunganishwa pamoja katika mti wao tena.
25 Ndugu zangu, ieleweni siri hii ya ukweli. Kweli hii itawasaidia ninyi mjue kuwa hamfahamu kila kitu. Kweli ni hii: Sehemu ya Israeli wamefanywa kuwa wakaidi, lakini hiyo itabadilika wasio Wayahudi, wengi, watakapokuja kwa Mungu. 26 Na hivyo ndivyo Israeli wote watakavyookolewa. Kama Maandiko yanavyosema,
“Mwokozi atakuja kutoka Sayuni;
atauondoa uovu kutoka kwa wazaliwa wa Yakobo.
27 Nami nitalifanya patano hili na watu wale
nitakapoziondoa dhambi zao.”(F)
28 Kwa sasa, Wayahudi wanaokataa kuzipokea Habari Njema wamekuwa adui wa Habari Njema. Hili limetokea kwa manufaa yenu ninyi msio Wayahudi. Lakini bado Wayahudi ni wateule wa Mungu, na anawapenda kwa sababu ya ahadi alizozifanya kwa baba zao. 29 Mungu habadili mawazo yake kuhusu watu anaowaita. Kamwe haamui kuzirudisha baraka alizokwisha kuwapa. 30 Wakati mmoja ninyi pia mlikataa kumtii Mungu. Lakini sasa mmeipokea rehema, kwa sababu Wayahudi walikataa kutii. 31 Na sasa wao ndiyo wanaokataa kutii, kwa sababu Mungu aliwaonesha ninyi rehema zake. Lakini hili limetokea ili nao pia waweze kupokea rehema kutoka kwake. 32 Mungu amemfungia kila mmoja katika gereza la kutokutii. Lakini amefanya hivi ili aweze kuonesha rehema yake kwa wote.
Sifa kwa Mungu
33 Ndiyo, utajiri wa Mungu ni mkuu sana! Hekima yake na ufahamu wake havina mwisho! Hakuna awezaye kuelezea yale Mungu anayoyaamua. Hayupo awezaye kuzielewa njia zake. 34 Kama Maandiko yanavyosema,
“Nani anaweza kuyajua yaliyo katika mawazo ya Bwana?
Nani anaweza kumshauri?”(G)
35 “Nani amewahi kumpa Mungu kitu chochote?
Mungu hadaiwi kitu chochote na mtu yeyote.”(H)
36 Ndiyo, Mungu ameviumba vitu vyote. Na kila kitu kinaendelea kuwepo kwa njia na kwa ajili yake. Utukufu uwe kwa Mungu milele yote! Amina.
Copyright © 2017 by Bible League International