Waefeso 2
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Kutoka Mauti hadi Uzima
2 Zamani mlikuwa wafu kiroho kwa sababu ya dhambi na mambo mliyotenda kinyume na Mungu. 2 Ndiyo, zamani maisha yenu yalijaa dhambi hizo. Mliishi kwa namna ya ulimwengu; mkimfuata mkuu wa nguvu za uovu[a] zilizo katika anga, roho hiyo hiyo inatenda kazi sasa ndani ya watu wasiomtii Mungu. 3 Tuliishi hivyo zamani, tukijaribu kuzifurahisha tamaa zetu za mwili. Tulitenda mambo ambayo miili na akili zetu zilitaka. Kama ilivyo kwa kila mtu ulimwenguni, tulistahili kuteseka kutokana na hasira ya Mungu kwa sababu ya jinsi tulivyokuwa.
4 Lakini Mungu ni mwingi wa rehema na anatupenda sana. 5 Tulikuwa wafu kiroho kwa sababu ya matendo maovu tuliyotenda kinyume naye. Lakini yeye alitupa maisha mapya pamoja na Kristo. (Mmeokolewa na neema ya Mungu.) 6 Ndiyo, ni kwa sababu sisi ni sehemu ya Kristo Yesu, ndiyo maana Mungu alitufufua pamoja naye kutoka kwa wafu na akatuketisha pamoja naye mbinguni. 7 Mungu alifanya hivi ili wema wake kwetu sisi tulio wa Kristo Yesu uweze kuonesha nyakati zote zijazo utajiri wa ajabu wa neema yake.
8 Nina maana ya kuwa mmeokolewa kwa neema kwa sababu mliweka imani yenu kwake.[b] Hamkujiokoa ninyi wenyewe; bali ni zawadi kutoka kwa Mungu. 9 Msijisifu kwa kuwa hamkuokolewa kutokana na matendo yenu. 10 Mungu ndiye aliyetufanya hivi tulivyo. Ametuumba wapya katika Kristo Yesu ili tutende mambo mema katika maisha yetu. Mambo aliyokwisha kutupangia.
Wamoja Katika Kristo
11 Hamkuzaliwa mkiwa Wayahudi. Ninyi ni watu ambao Wayahudi huwaita “Wasiotahiriwa”,[c] na wao wakijiita “Waliotahiriwa” (Tohara yao ni ile inayofanyika kwenye miili yao kwa mikono ya binadamu.) 12 Kumbukeni ya kwamba zamani hamkuwa na Kristo. Hamkuwa raia wa Israeli na hamkujua kuhusu mapatano ya maagano[d] ambayo Mungu aliyaweka kwa watu wake. Hamkuwa na tumaini na hamkumjua Mungu. 13 Lakini sasa mmeungana na Kristo Yesu. Ndiyo, wakati fulani hapo zamani mlikuwa mbali na Mungu, lakini sasa mmeletwa karibu naye kupitia sadaka ya damu ya Kristo.
14 Kristo ndiye sababu ya amani yetu. Yeye ndiye aliyetufanya sisi Wayahudi nanyi msio Wayahudi kuwa wamoja. Tulitenganishwa na ukuta wa chuki uliokuwa kati yetu, lakini Kristo aliubomoa. Kwa kuutoa mwili wake mwenyewe, 15 Kristo aliisitisha sheria pamoja na kanuni na amri zake nyingi. Kusudi lake lilikuwa ni kuyafanya makundi mawili yawe wanadamu wamoja waliounganishwa naye. Kwa kufanya hivi alikuwa analeta amani. 16 Kupitia msalaba Kristo alisitisha uhasama kati ya makundi mawili. Na baada ya makundi haya kuwa mwili mmoja, alitaka kuwapatanisha wote tena kwa Mungu. Alifanya hivi kwa kifo chake msalabani. 17 Kristo alikuja na kuwaletea ujumbe wa amani ninyi msio Wayahudi mliokuwa mbali na Mungu. Na aliwaletea pia ujumbe huo wa amani watu waliokaribu na Mungu. 18 Ndiyo, kupitia Kristo sisi sote tuna haki ya kumjia Baba katika Roho mmoja.
19 Hivyo ninyi msio Wayahudi si wageni wala wahamiaji, lakini ninyi ni raia pamoja na watakatifu wa Mungu. Ninyi ni wa familia ya Mungu. 20 Ninyi mnaoamini ni kama jengo linalomilikiwa na Mungu. Jengo hilo limejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii. Kristo Yesu mwenyewe ndiye jiwe kuu la muhimu sana[e] katika jengo hilo. 21 Jengo lote limeunganishwa katika Kristo, naye hulikuza na kuwa hekalu[f] takatifu katika Bwana. 22 Na katika Kristo mnajengwa pamoja na watu wake wengine. Mnafanywa kuwa makazi ambapo Mungu anaishi katika Roho.
Footnotes
- 2:2 mkuu wa nguvu za uovu Tazama Shetani katika Orodha ya Maneno.
- 2:8 kwa … kwake Au “kwa sababu ya uaminifu wake”.
- 2:11 Wasiotahiriwa Watu wasio na alama ya tohara kama Wayahudi.
- 2:12 maagano Maagano au ahadi maalum ambazo Mungu alizitoa nyakati tofauti kwa watu katika Agano la Kale. Tazama Agano (Makubaliano) katika Orodha ya Maneno.
- 2:20 jiwe kuu la muhimu sana Kwa maana ya kawaida, “Jiwe na msingi kwenye pembe”. Jiwe la kwanza na la muhimu sana katika jengo.
- 2:21 hekalu Nyumba ya Mungu, mahali ambapo watu wa Mungu humwabudu. Hapa, inamaanisha kuwa waamini ndiyo hekalu la kiroho ambamo Mungu anaishi.
Copyright © 2017 by Bible League International