Waebrania 2
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Wokovu Wetu ni Mkuu Kuliko Sheria
2 Hivyo tunapaswa kuwa makini zaidi kuzingatia yale tuliyofundishwa. Tunapaswa kuwa makini ili tusiondolewe polepole kutoka katika njia iliyo ya kweli. 2 Fundisho kwamba Mungu alizungumza kupitia malaika limedhihirishwa kuwa ni la kweli. Na kila mara watu wake walipotenda jambo kinyume na fundisho lake, waliadhibiwa kwa yale waliyofanya. Waliadhibiwa walipoacha kutii fundisho hilo. 3 Hivyo kwa hakika hata nasi tutaadhibiwa kama hatutauzingatia wokovu mkuu tulionao. Alikuwa ni Bwana Yesu aliyewaambia watu kwa mara ya kwanza juu ya wokovu huo. Na wale waliomsikiliza walithibitisha kwetu kuwa yale mambo yalikuwa ni kweli. 4 Mungu alithibitisha hayo pia kwa kutumia ishara, maajabu, na aina zingine zote za miujiza. Na alithibitisha hayo kwa kuwapa watu vipawa tofauti kwa njia ya Roho Mtakatifu kwa namna ile aliyotaka.
Kristo Akawa Kama Watu Ili Awaokoe
5 Mungu hakuwachagua malaika wawe watawala juu ya ulimwengu mpya unaokuja. Ulimwengu huo ujao ni ndiyo ambao tumekuwa tukiuzungumzia. 6 Imeandikwa mahali fulani katika Maandiko:
“Kwa nini watu ni muhimu sana kwako?
Kwa nini hata unafikiri juu yao?
Kwa nini unamjali mwana wa mwanadamu?[a]
Je, yeye ni muhimu kiasi hicho?
7 Kwa muda mfupi ulimfanya awe chini kuliko malaika.
Ukamvisha taji yenye utukufu na heshima.
8 Ukaweka kila kitu chini ya udhibiti wake.”[b](A)
Kama Mungu aliweka vitu vyote chini ya udhibiti wake, basi hakikuwepo chochote kilichoachwa ambacho hakukitawala. Lakini bado hatujamwona akitawala juu ya vyote. 9 Kwa kipindi kifupi Yesu aliwekwa chini kuliko malaika, lakini sasa tunamwona akiwa amevaa taji ya utukufu na heshima kwa sababu aliteseka na kufa. Kwa sababu ya neema ya Mungu, Yesu alikufa kwa ajili ya kila mmoja.
10 Mungu aliyeumba vitu vyote na ambaye kwa utukufu wake vitu vyote vipo; alitaka watu wengi wawe watoto wake na kuushiriki utukufu wake. Hivyo alifanya yale aliyohitaji kuyafanya. Alimkamilisha yeye anayewaongoza watu hao kuuelekea wokovu. Kwa njia ya mateso yake Mungu alimfanya Yesu kuwa Mwokozi mkamilifu.
11 Yesu, ambaye anawafanya watu kuwa watakatifu, na wale wanaofanywa kuwa watakatifu wanatoka katika familia moja. Hivyo haoni aibu kuwaita kaka na dada zake. 12 Anasema,
“Mungu, nitawaeleza kaka na dada zangu habari zako.
Mbele za watu wako wote nitaziimba sifa zako.”(B)
13 Pia anasema,
“Nitamwamini Mungu.”(C)
Na pia anasema,
“Nipo hapa, na pamoja ni wapo watoto
niliopewa na Mungu.”(D)
14 Watoto hawa ni watu walio na miili ya damu na nyama. Hivyo Yesu mwenyewe akawa kama wao na akapata uzoefu ule ule waliokuwa nao. Yesu alifanya hivi ili, kwa kufa kwake, aweze kumharibu yeye aliye na nguvu ya mauti, Ibilisi. 15 Yesu akawa kama watu hawa na akafa ili aweze kuwaweka huru. Walikuwa kama watumwa maisha yao yote kwa sababu ya kuogopa kwao kifo. 16 Kwa uwazi, siyo malaika ambao Yesu huwasaidia. Yeye huwasaidia watu waliotoka kwa Ibrahimu. 17 Kwa sababu hii, Yesu alifanyika kama sisi, kaka na dada zake kwa kila namna. Akawa kama sisi ili aweze kuhudumu kwa niaba yetu mbele za Mungu wa kuhani mkuu aliye mwaminifu na mwenye rehema. Ndipo angetoa sadaka ya kuziondoa dhambi za watu. 18 Na sasa anaweza kuwasaidia wale wanaojaribiwa. Yuko radhi kuwasaidia kwa sababu yeye mwenyewe aliteseka na alijaribiwa.
Footnotes
- 2:6 mwana wa mwanadamu Hii inaweza kumaanisha mwanadamu yeyote, lakini jina “Mwana wa Mtu” (tazama Mwana wa Mtu katika Orodha ya Maneno) mara kwa mara imetumika kumaanisha Yesu, ambaye alionesha yale Mungu aliyokusudia watu wote wawe.
- 2:8 chini ya udhibiti wake Kwa maana ya kawaida, “kuweka chini ya miguu”.
Copyright © 2017 by Bible League International