Waebrania 12
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Sisi Pia Tuufuate Mfano wa Yesu
12 Tunao hawa watu mashuhuri wakituzunguka kama mifano kwetu. Maisha yao yanatueleza imani ni nini. Hivyo, nasi pia, tunapaswa kufanya mashindano yaliyo mbele yetu na kamwe tusikate tamaa. Tunapaswa kuondoa katika maisha yetu kitu chochote kitakachotupunguzia mwendo pamoja na dhambi zinazotufanya tutoke kwenye mstari mara kwa mara. 2 Hatupaswi kuacha kumwangalia Yesu. Yeye ndiye kiongozi wa imani yetu, na ndiye anayeikamilisha imani yetu. Aliteseka hadi kufa msalabani. Lakini aliikubali aibu ya msalaba kama kitu kisicho na maana kwa sababu ya furaha ambayo angeiona ikimngojea. Na sasa ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. 3 Mfikirie Yesu. Kwa uvumilivu alistahimili matusi ya hasira ya watenda dhambi waliokuwa wakiwapigia kelele. Mfikirie yeye ili usikate tamaa na kuacha kujaribu.
Mungu ni Kama Baba
4 Mnashindana na dhambi, lakini bado hamjamwaga damu hata kuutoa uhai wenu katika mashindano hayo. 5 Ninyi ni watoto wa Mungu, naye huzungumza maneno ya faraja kwenu. Labda mmeyasahau maneno haya:
“Mwanangu, wakati Mungu anapokurekebisha,
zingatia na usiache kujaribu.
6 Bwana humrekebisha kila anayempenda;
humpa adhabu kila anayemkubali kama mwana wake.”(A)
7 Hivyo muyapokee mateso kama adhabu ya baba. Mungu hufanya mambo haya kwenu kama baba anavyowarekebisha watoto wake. Mnajua kuwa watoto wote hurekebishwa na baba zao. 8 Hivyo, kama hukupata marekebisho ambayo kila mtoto anapaswa kuyapata, wewe siyo mtoto wa kweli na hakika wewe siyo wa Mungu. 9 Sisi wote tulikuwa na baba wa hapa duniani walioturekebisha, na tuliwaheshimu. Ni muhimu zaidi basi kwamba tunapaswa kuyapokea marekebisho kutoka kwa Baba wa roho zetu. Tukifanya hivyo, tutakuwa na uzima. 10 Baba zetu wa duniani waliturekebisha kwa muda mfupi katika njia waliyofikiri ilikuwa bora zaidi. Lakini Mungu huturekebisha sisi ili atusaidie tuweze kuwa watakatifu kama yeye. 11 Hatufurahii marekebisho tunapokuwa tunayapata. Yanauma. Lakini baadaye, baada ya kujifunza somo kutokana na hayo, tutaifurahia amani itakayokuja kwa njia ya kufanya yaliyo sahihi.
Muwe Makini Jinsi Mnavyoishi
12 Mmekuwa dhaifu, hebu mjitie nguvu tena. 13 Muishi katika njia iliyo sahihi ili muweze kuokolewa na udhaifu wenu hautawasababisha ninyi kupotea.
14 Jitahidini kuishi kwa amani na kila mtu. Na mjitahidi kuyaweka mbali na dhambi maisha yenu. Yeyote ambaye maisha yake siyo matakatifu hawezi kumwona Bwana. 15 Muwe makini ili mtu asije akakosa kuipata neema ya Mungu. Muwe makini ili asiwepo atakayepoteza imani yake na kuwa kama gugu chungu linalomea miongoni mwenu. Mtu wa jinsi hiyo anaweza kuharibu kundi lenu lote. 16 Muwe makini ili asiwepo yeyote atakayefanya dhambi ya uzinzi au kushindwa kumheshimu Mungu moyoni kama alivyofanya Esau. Kama kijana mkubwa katika nyumba ya babaye, Esau angerithi sehemu kubwa ya vitu kutoka kwa baba yake. Lakini akauza kila kitu kwa mlo mmoja tu. 17 Mnakumbuka kwamba baada ya Esau kufanya hivi, akataka kupata baraka za baba yake. Akaitamani sana baraka ile kiasi kwamba akalia. Lakini baba yake akakataa kumpa baraka hiyo, kwa sababu Esau hakupata njia ya kubadili yale aliyotenda.
18 Ninyi ni watu wa Mungu, kama watu wa Israeli walipofika katika Mlima Sinai. Lakini hamjaufikia mlima halisi wa kuweza kushikwa. Mlima huo haupo kama ule waliouona, uliokuwa ukiwaka moto na kufunikwa na giza, utusitusi na dhoruba. 19 Haipo sauti ya tarumbeta au sauti iliyoyasema maneno kama hayo waliyoyasikia. Walipoisikia sauti, wakasihi kamwe wasisikie neno lingine. 20 Hawakutaka kusikia amri: “Kama chochote, hata mnyama, akigusa mlima, lazima kiuawe kwa kupigwa mawe.”(B) 21 Kile walichoona kilikuwa cha kutisha kiasi kwamba Musa akasema, “Natetemeka kwa hofu.”(C)[a]
22 Lakini mmeufikia Mlima Sayuni, kwenye mji wa Mungu aliye hai, Yerusalemu wa mbinguni.[b] Mmefika mahali ambapo maelfu wa malaika wamekusanyika kusherehekea. 23 Mmefika katika kusanyiko la watoto wazaliwa wa kwanza wa Mungu. Majina yao yameandikwa mbinguni. Mmemfikia Mungu, hakimu wa watu wote. Na mmefika kwenye roho za watu wema ambao wamekamilishwa. 24 Mmemfikia Yesu; yeye aliyelileta kutoka kwa Mungu agano jipya kwenda kwa watu wake. Mmefika kwenye damu iliyonyunyizwa[c] ambayo inasema habari za mema zaidi kuliko damu ya Habili.
25 Muwe makini na msijaribu kupuuza kusikiliza Mungu anaposema. Watu wale walipuuza kumsikiliza yeye alipowaonya hapa duniani. Nao hawakuponyoka. Sasa Mungu anasema kutoka mbinguni. Hivyo sasa itakuwa vibaya zaidi kwa wale watakaopuuza kumsikiliza yeye. 26 Alipozungumza pale mwanzoni, sauti yake iliitetemesha dunia. Lakini sasa ameahidi, “Kwa mara nyingine tena nitaitetemesha dunia, lakini pia nitazitetemesha mbingu.”(D) 27 Maneno “Kwa mara nyingine” yanatuonyesha kwa uwazi kwamba kila kitu kilichoumbwa kitaangamizwa; yaani, vitu vinavyoweza kutetemeshwa. Na ni kile tu kisichoweza kutetemeshwa kitakachobaki.
28 Hivyo tunahitajika kuwa na shukrani kwa sababu tunao ufalme ambao hauwezi kutetemeshwa. Na kwa sababu sisi ni watu wa shukrani, tunahitajika kumwabudu Mungu kwa njia itakayompendeza yeye. Tunahitajika kufanya hivi kwa heshima na hofu, 29 kwa sababu “Mungu wetu yuko kama moto unaoweza kutuangamiza sisi.”(E)
Copyright © 2017 by Bible League International