Waebrania 11
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Imani
11 Imani inaleta uthabiti wa mambo tunayoyatarajia. Ni uthibitisho wa yale tusiyoweza kuyaona. 2 Mungu alifurahishwa na watu walioishi muda mrefu uliopita kwa sababu walikuwa na imani ya namna hii.
3 Imani hutusaidia sisi kufahamu kwamba Mungu aliumba ulimwengu wote kwa amri yake. Hii inamaanisha kwamba vitu tunavyoviona viliumbwa kwa kitu kisichoonekana.
4 Kaini na Habili wote walitoa sadaka kwa Mungu. Lakini Habili alitoa sadaka bora zaidi kwa Mungu kwa sababu alikuwa na imani. Mungu akasema alifurahishwa na kile alichotoa Habili. Na hivyo Mungu akamwita kuwa mtu mwema kwa sababu alikuwa na imani. Habili akafariki, lakini kupitia imani yake bado anazungumza.
5 Henoko alitwaliwa kutoka duniani, hivyo kamwe yeye hajafariki. Maandiko yanatueleza kwamba kabla ya kuchukuliwa, alikuwa mtu aliyempendeza Mungu. Baadaye, hayupo yeyote aliyejua kule alikokuwa, kwa sababu Mungu alimchukua Henoko ili awe pamoja naye. Haya yote yakatokea kwa vile alikuwa na imani. 6 Bila kuwa na imani hakuna anayeweza kumfurahisha Mungu. Yeyote anayemjia Mungu anatakiwa kuamini kwamba yeye ni hakika na kwamba anawalipa wale ambao kwa uaminifu wanajitahidi kumtafuta.
7 Nuhu alionywa na Mungu juu ya mambo ambayo hakuwa ameyaona bado. Lakini alikuwa na imani na heshima kwa Mungu, hivyo akaijenga meli kubwa ili kuiokoa familia yake. Kwa imani yake, Nuhu alionesha kwamba ulimwengu ulikuwa umekosea. Na akawa ni mmoja wa wale waliohesabiwa haki na Mungu kwa njia ya imani.
8 Mungu alimwita Ibrahimu kusafiri kwenda sehemu ingine aliyoahidi kumpa. Ibrahimu hakujua hiyo sehemu ingine ilikuwa wapi. Lakini alimtii Mungu na akaanza kusafiri kwa sababu alikuwa na imani. 9 Ibrahimu akaishi katika nchi ambayo Mungu aliahidi kumpa. Akaishi humo kama mgeni tu asiyekuwa mwenyeji. Alifanya hivi kwa sababu alikuwa na imani. Akaishi katika mahema pamoja na Isaka na Yakobo, ambao pia walipokea ahadi ile ile kutoka kwa Mungu. 10 Ibrahimu alikuwa anaungoja mji[a] ambao ulikuwa na misingi halisi. Alikuwa anaungoja mji ulibuniwa na kujengwa na Mungu.
11 Sara hakuwa na uwezo wa kupata watoto, na Ibrahimu alikuwa amezeeka sana. Lakini alikuwa anamwamini Mungu, akimwamini kuwa anaweza kutenda yale aliyoahidi. Hivyo Mungu akawawezesha kupata watoto. 12 Ibrahimu alikuwa amezeeka sana karibu ya kufa. Lakini kupitia kwa mtu huyo mmoja vikaja vizazi vingi kama zilivyo nyota za angani. Hivyo watu wengi wakaja kutoka kwake wakiwa kama punje za mchanga katika ufukwe wa bahari.
13 Watu hawa wote mashuhuri wakaendelea kuishi kwa imani hadi walipofariki. Hawakuwa wamepata mambo ambayo Mungu aliwaahidi watu wake. Lakini walikuwa na furaha kuona tu kwamba ahadi hizi zilikuwa zinakuja kwa mbali siku zijazo. Waliukubali ukweli kwamba wao walikuwa kama wageni na wasafiri hapa duniani. 14 Watu wanapolikubali jambo la namna hiyo, wanaonesha kuwa wanaingojea nchi itakayokuwa yao wenyewe. 15 Kama wangekuwa wanaifikiria nchi walikotoka, wangekuwa wamerejea. 16 Lakini walikuwa wanaingoja nchi iliyo bora zaidi, nchi ya mbinguni. Hivyo Mungu haoni aibu kuitwa Mungu wao. Naye amewaandalia mji.
17-18 Mungu aliijaribu imani ya Ibrahimu. Mungu alimtaka amtoe Isaka kama sadaka. Ibrahimu akatii kwa sababu alikuwa na imani. Tayari alikuwa na ahadi kutoka kwa Mungu. Na Mungu tayari alikuwa amekwishamwambia, “Ni kupitia kwa Isaka kwamba vizazi vyako watakuja.”(A) Lakini Ibrahimu alikuwa tayari kumtoa mwana wake wa pekee. Alifanya hivi kwa sababu alikuwa na imani. 19 Aliamini kwamba Mungu angeweza kuwafufua watu kutoka kifoni. Na hakika, Mungu alipomzuia Ibrahimu katika kumuua Isaka, ilikuwa ni kama vile alimpata tena kutoka kifoni.
20 Isaka akayabariki maisha ya mbeleni ya Yakobo na Esau. Alifanya hivyo kwa sababu alikuwa na imani. 21 Na Yakobo, pia kwa vile alikuwa na imani, alimbariki kila mmoja wa wana wa Yusufu. Alifanya haya wakati alipokuwa akifa, akaiegemea fimbo yake akimwabudu Mungu.
22 Na Yusufu alipokuwa karibu amefariki, alizungumza kuhusu watu wa Israeli kuondoka Misri. Na aliwaambia yale waliyotakiwa kuufanyia mwili wake. Alifanya haya kwa sababu alikuwa na imani.
23 Na mama na baba wa Musa wakaona kwamba alikuwa ni mtoto mzuri hivyo wakamficha kwa miezi mitatu baada ya kuzaliwa kwake. Hili lilikuwa kinyume na agizo la mfalme. Lakini hawakuogopa kwa sababu walikuwa na imani.
24-25 Musa akakua na akawa mwanaume. Akakataa kuitwa mwana wa binti Farao. Akachagua kutokujifurahisha katika raha na dhambi zinazodumu kwa muda mfupi tu. Badala yake, akachagua kuteseka pamoja na watu wa Mungu. Alifanya hivi kwa sababu alikuwa na imani. 26 Alifikiri kuwa ni bora kuteseka kwa ajili ya Masihi kuliko kuwa na hazina zote za Misri. Alikuwa anaisubiri malipo ambayo Mungu angempa.
27 Musa akaondoka Misri kwa sababu alikuwa na imani. Hakuiogopa hasira ya mfalme. Aliendelea kuwa jasiri kama vile angemwona Mungu ambaye hakuna mtu mwingine angeweza kumwona. 28 Na kwa sababu alikuwa na imani, Musa akaandaa mlo wa Pasaka. Na akanyunyiza damu ya mwanakondoo katika miimo ya milango ya watu wake, ili kwamba malaika wa kifo[b] asiwaue wazaliwa wao wa kwanza wa kiume.
29 Na watu wa Mungu wote wakatembea kuvuka Bahari ya Shamu kama vile ilikuwa ni ardhi kavu. Waliweza kufanya hivi kwa sababu walikuwa na imani. Lakini wakati Wamisri walipojaribu kuwafuata, wote wakazama majini.
30 Na kuta za Yeriko zilianguka kwa ajili ya imani ya watu wa Mungu. Walitembea kuuzunguka ukuta kwa siku saba, na kisha kuta zikaanguka.
31 Na Rahabu, yule kahaba, aliwakaribisha wapelelezi wa Kiisraeli kama marafiki. Na kwa sababu ya imani yake, hakuuawa pamoja na wale waliokataa kutii.
32 Je, nahitaji niwape mifano zaidi? Sina muda wa kutosha kuwaeleza kuhusu Gidioni, Baraki, Samsoni, Yefta, Daudi, Samweli na manabii. 33 Wote walikuwa na imani kuu. Na kwa njia ya imani hiyo wakaziangusha falme. Wakafanya kilichokuwa sahihi, na Mungu akawasaidia katika njia alizoahidi. Kwa imani zao watu wengine waliifunga midomo ya simba. 34 Na wengine waliweza kuizuia miali ya moto. Wengine wakaepuka katika kuuawa kwa upanga. Wengine waliokuwa dhaifu wakafanywa wenye nguvu. Wakawa na nguvu katika vita na kuyaangusha majeshi mengine. 35 Walikuwepo wanawake waliowapoteza wapendwa wao lakini wakawapata tena walipofufuliwa kutoka wafu. Wengine waliteswa lakini wakakataa kuukubali uhuru wao. Walifanya hivi ili waweze kufufuliwa kutoka kifoni kuingia katika maisha bora zaidi. 36 Wengine walichekwa na kupigwa. Wengine walifungwa na kutiwa magerezani. 37 Waliuawa kwa mawe. Walikatwa vipande viwili. Waliuawa kwa panga. Mavazi pekee wengine wao waliyokuwa nayo yalikuwa ni ngozi za kondoo au za mbuzi. Walikuwa maskini, waliteswa, na kutendewa mabaya na wengine. 38 Ulimwengu haukustahili kuwa na watu wakuu na waaminifu kama hawa. Hawa waliweza kuzunguka jangwani na milimani, wakiishi katika mapango na mashimo ardhini.
39 Mungu alifurahishwa nao wote kwa sababu ya imani zao. Lakini hakuna hata mmoja wao aliyepokea ahadi ya Mungu. 40 Mungu alikusudia kitu bora zaidi kwa ajili yetu. Alitaka kutukamilisha sisi. Hakika, pia alitaka watu hawa wakuu wakamilishwe, lakini siyo kabla ya sisi wote kuzifurahia baraka pamoja.
Copyright © 2017 by Bible League International