Ufunuo 4
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Yohana Aiona Mbingu
4 Kisha nikatazama, na mbele yangu ulikuwepo mlango uliokuwa wazi mbinguni. Na nikasikia sauti iliyosema nami mwanzoni. Ilikuwa sauti iliyosikika kama tarumbeta. Ilisema, “Njoo huku juu, nitakuonesha yale ambayo ni lazima yatokee baada ya hili.” 2 Ghafla Roho akanichukua, na huko mbinguni kilikuwepo kiti cha enzi na mmoja amekaa juu yake. 3 Aliyekikalia alikuwa mzuri kama mawe ya thamani, kama yaspi na karneli. Pande zote kuzunguka kiti cha enzi kulikuwa upinde wa mvua wenye rangi kama zumaridi.
4 Vilikuwepo viti vingine vya enzi ishirini na nne kuzunguka kiti cha enzi vilivyokaliwa na wazee ishirini na nne. Wazee walikuwa wamevaa nguo nyeupe na taji za dhahabu vichwani mwao. 5 Mianga na ngurumo za radi vilitoka katika kiti cha enzi. Mbele ya kiti cha enzi zilikuwepo taa saba zikiwaka, ambazo ndizo Roho saba za Mungu. 6 Pia mbele ya kiti cha enzi kilikuwepo kitu kilichoonekana kama bahari ya kioo, iiliyo angavu sana.
Mbele ya kiti cha enzi na kukizunguka pande zake zote walikuwepo viumbe wenye uhai wanne. Walikuwa na macho kila mahali. 7 Kiumbe wa kwanza alikuwa kama simba. Wa pili alikuwa kama fahali. Wa tatu alikuwa na uso kama wa mwanadamu. Wa nne alikuwa kama tai anayeruka. 8 Kila mmoja wa hawa wenye uhai wanne alikuwa na mabawa sita. Walikuwa na macho kila mahali, ndani na nje. Usiku na mchana hawaachi kusema:
“Mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu ni Bwana Mungu Mwenye nguvu zote.
Daima amekuwepo, yupo na anakuja.”
9 Wenye uhai hawa wanne walikuwa wanampa utukufu, heshima na shukrani yule anayekaa kwenye kiti cha enzi, anayeishi milele na milele. Na kila wakati walifanya hivyo, 10 wazee ishirini na nne waliinama mbele ya[a] yule anayekaa kwenye kiti cha enzi. Wanamwabudu anayeishi milele na milele. Wanaweka taji zao mbele ya kiti cha enzi na kusema:
11 “Bwana wetu na Mungu!
Unastahili kupokea utukufu, heshima na nguvu.
Uliumba vitu vyote.
Kila kinachoishi kiliumbwa kwa sababu ulitaka.”
Footnotes
- 4:10 waliinama mbele ya Yaani, “walimsujudia”.
Copyright © 2017 by Bible League International