Add parallel Print Page Options

Malaika Wenye Mapigo ya Mwisho

15 Ndipo nikaona ajabu nyingine mbinguni, ilikuwa kubwa na ya kushangaza. Walikuwepo malaika saba wenye mapigo saba. Haya ni mapigo ya mwisho kwa sababu baada ya haya, ghadhabu ya Mungu itakuwa imekwisha.

Niliona kama bahari ya kioo iliyochanganyikana na moto. Wale wote waliomshinda mnyama na sanamu yake na namba ya jina lake walikuwa wamesimama kando ya bahari. Watu hawa walikuwa na vinubi walivyopewa na Mungu. Waliuimba wimbo wa Musa, mtumishi wa Mungu na wimbo wa Mwanakondoo:

“Mambo unayotenda ni makuu na ya kushangaza,
    Bwana Mungu Mwenye Nguvu.
Njia zako ni sahihi na za kweli,
    mtawala wa mataifa.
Watu wote watakucha wewe, Ee Bwana.
    Watu wote watalisifu jina lako.
    Mtakatifu ni wewe peke yako.
Watu wote watakuja na kusujudu mbele yako,
    kwa sababu ni dhahiri kuwa wewe hutenda yaliyo haki.”

Baada ya hili nikaona hekalu, mahali patakatifu pa Mungu[a] mbinguni. Likiwa wazi; kisha malaika saba wenye mapigo saba wakatoka nje ya hekalu. Walikuwa wamevaa kitani safi inayong'aa. Wamevaa mikanda mipana ya dhahabu vifuani mwao. Kisha mmoja wa viumbe wenye uhai wanne akawapa malaika bakuli saba za dhahabu. Bakuli zilikuwa zimejaa ghadhabu ya Mungu, aishiye milele na milele. Hekalu lilikuwa limejaa moshi uliotoka katika utukufu na nguvu ya Mungu. Hakuna ambaye angeweza kuingia hekaluni mpaka mapigo saba ya malaika saba yamemalizika.

Footnotes

  1. 15:5 mahali patakatifu pa Mungu Kwa maana ya kawaida, “Hema ya Ushuhuda”. Tazama Hema Takatifu katika Orodha ya Maneno. Soma Kut 25:8-22.