Mathayo 15
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Sheria ya Mungu na Desturi za Kibinadamu
(Mk 7:1-23)
15 Kisha baadhi ya Mafarisayo na walimu wa sheria kutoka Yerusalemu walimjia Yesu na kumwuliza, 2 “Kwa nini wafuasi wako hawatii desturi tulizorithi kutoka kwa viongozi wetu wakuu walioishi hapo zamani? Wafuasi wako hawanawi mikono kabla ya kula!”
3 Yesu akajibu, “Na kwa nini mnakataa kutii amri ya Mungu ili muweze kuzifuata desturi zenu? 4 Mungu alisema, ‘Ni lazima umtii baba na mama yako.’(A) Na Mungu alisema pia kuwa, ‘Kila anayemnenea vibaya mama au baba yake lazima auawe.’(B) 5 Lakini mnafundisha kuwa mtu anaweza kumwambia baba au mama yake, ‘Nina kitu ninachoweza kukupa kukusaidia, Lakini sitakupa, bali nitampa Mungu.’ 6 Mnawafundisha kutowatii baba zao. Hivyo mnafundisha kuwa si muhimu kufanya kile alichosema Mungu. Mnadhani ni muhimu kufuata mila na desturi zenu mlizonazo. 7 Enyi wanafiki! Isaya alikuwa sahihi alipozungumza kwa niaba ya Mungu kuhusu ninyi aliposema:
8 ‘Watu hawa wananiheshimu kwa maneno tu,
lakini mimi si wa muhimu kwao.
9 Ibada zao kwangu hazina maana.
Wanafundisha kanuni za kibinadamu tu.’”(C)
10 Yesu akawaita watu. Akasema, “Sikieni na mwelewe nitakachosema. 11 Si chakula kinachoingia mdomoni kinachomtia mtu unajisi,[a] bali kile kinachomtoka mdomoni mwake.” 12 Kisha wafuasi wakamjia na kumwuliza, “Unajua kuwa Mafarisayo wamekasirika kutokana na yale uliyosema?”
13 Yesu akajibu, “Kila mti ambao haukupandwa na Baba yangu wa mbinguni utang'olewa. 14 Kaeni mbali na Mafarisayo. Wanawaongoza watu, lakini ni sawa na wasiyeona wanaowaongoza wasiyeona wengine. Na kama asiyeona akimwongoza asiyeona mwingine, wote wawili wataangukia shimoni.”
15 Petro akasema, “Tufafanulie yale uliyosema awali kuhusu kile kinachowatia watu najisi.”
16 Yesu akasema, “Bado mna matatizo ya kuelewa? 17 Hakika mnajua kuwa vyakula vyote vinavyoingia kinywani huenda tumboni. Kutoka huko hutoka nje ya mwili. 18 Lakini mambo mabaya ambayo watu wanasema kwa vinywa vyao hutokana na mawazo yao. Na hayo ndiyo yanayoweza kumtia mtu unajisi. 19 Mambo mabaya haya yote huanzia akilini: mawazo maovu, mauaji, uzinzi, uasherati, wizi, uongo, na matukano. 20 Haya ndiyo mambo yanayowatia watu unajisi. Kula bila kunawa mikono hakuwezi kuwafanya watu wasikubaliwe na Mungu.”
Yesu Amsaidia Mwanamke Asiye Myahudi
(Mk 7:24-30)
21 Kutoka pale, Yesu alikwenda maeneo ya Tiro na Sidoni. 22 Mwanamke Mkanaani kutoka eneo hilo akatokea na kuanza kupaza sauti, “Bwana, Mwana wa Daudi, tafadhali nisaidie! Binti yangu ana pepo ndani yake, na anateseka sana.”
23 Lakini Yesu hakumjibu. Hivyo wanafunzi wake wakamwendea Yesu na kumwambia, “Mwambie aondoke, anaendelea kupaza sauti na hatatuacha.”
24 Yesu akajibu, “Mungu alinituma niwasaidie kondoo wa Mungu waliopotea, watu wa Israeli.”[b]
25 Ndipo mwanamke alikuja mahali alipokuwa Yesu na kuinama mbele yake. Akasema, “Bwana, nisaidie!”
26 Akamjibu kwa kumwambia, “Si sahihi kuwapa mbwa mkate wa watoto.”
27 Mwanamke akasema, “Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula vipande vya chakula vinavyoanguka kutoka kwenye meza za mabwana zao.”
28 Kisha Yesu akamjibu, “Mwanamke, una imani kuu! Utapata ulichoomba.” Wakati huo huo binti wa yule mwanamke akaponywa.
Yesu Awaponya Watu Wengi
29 Kisha Yesu akatoka pale na kwenda pwani ya Ziwa Galilaya. Alipanda vilima na akaketi chini.
30 Kundi kubwa la watu likamwendea. Walileta watu wengine wengi waliokuwa wagonjwa na kuwaweka mbele yake. Walikuwepo watu wasioweza kutembea, wasiyeona, walemavu wa miguu, wasiyesikia na wengine wengi. 31 Watu walishangaa walipoona kuwa waliokuwa wasiyesema walianza kusema, walemavu wa miguu waliponywa, waliokuwa hawawezi kutembea waliweza kutembea, wasiyeona waliweza kuona. Kila mtu alimshukuru Mungu wa Israeli kwa hili.
Yesu Awalisha Watu Zaidi ya 4,000
(Mk 8:1-10)
32 Kisha Yesu akawaita wafuasi wake na kuwaambia, “Ninawaonea huruma watu hawa. Wamekuwa pamoja nami kwa siku tatu, na sasa hawana chakula. Sitaki niwaache waende wakiwa na njaa. Wanaweza kuzimia njiani wanaporudi nyumbani.”
33 Wafuasi wakamwuliza Yesu, “Tutapata wapi mikate ya kutosha kuwalisha watu wote hawa? Tuko nyikani mbali ni miji.”
34 Yesu akawauliza, “Mna mikate mingapi?”
Wakamjibu, “Tuna mikate saba na samaki wadogo wachache.”
35 Yesu akawaambia watu waketi chini. 36 Akaichukua mikate saba na samaki. Akamshukuru Mungu kwa sababu ya chakula. Akaigawa vipande vipande, akawapa wafuasi wake na wafuasi wakawapa watu chakula. 37 Watu wote walikula mpaka wakashiba. Baada ya hili, wafuasi walijaza vikapu saba kwa vipande vya chakula vilivyosalia ambavyo havikuliwa. 38 Walikuwepo wanaume 4,000 pale waliokula. Walikuwepo pia wanawake na watoto. 39 Baada ya wote kula, Yesu akawaambia watu wanaweza kwenda nyumbani. Alipanda mashua na kwenda eneo la Magadani.
Copyright © 2017 by Bible League International