Matendo 3
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Petro Amponya Kiwete
3 Siku moja Petro na Yohana walikwenda eneo la Hekalu saa tisa mchana, muda wa kusali na kuomba Hekaluni kama ilivyokuwa desturi. 2 Walipokuwa wanaingia katika eneo la Hekalu, mtu aliyekuwa mlemavu wa miguu maisha yake yote alikuwa amebebwa na baadhi ya rafiki zake waliokuwa wanamleta Hekaluni kila siku. Walimweka pembezoni mwa mojawapo ya Malango nje ya Hekalu. Lango hilo liliitwa Lango Zuri. Na mtu huyo alikuwa akiwaomba pesa watu waliokuwa wanaingia Hekaluni. 3 Siku hiyo alipowaona Petro na Yohana wakiingia eneo la Hekalu, aliwaomba pesa.
4 Petro na Yohana, walimtazama mtu huyo, wakamwambia, “Tutazame!” 5 Akawatazama akitumaini kuwa wangempa pesa. 6 Lakini Petro akasema, “Sina fedha wala dhahabu yoyote, lakini nina kitu kingine ninachoweza kukupa. Katika jina la Yesu Kristo wa Nazareti simama na utembee!”
7 Kisha Petro akamshika mkono wake wa kulia, akamnyenyua na kumsimamisha. Ndipo nyayo na vifundo vyake vikatiwa nguvu papo hapo. 8 Akaruka juu, akasimama kwa miguu yake na akaanza kutembea. Akaingia ndani ya eneo la Hekalu pamoja nao huku akitembea na kurukaruka akimsifu Mungu. 9-10 Watu wote walimtambua. Walimjua kuwa ni mlemavu wa miguu ambaye mara nyingi huketi kwenye Lango Zuri la Hekalu akiomba pesa. Lakini sasa walimwona anatembea na kumsifu Mungu. Walishangaa na hawakuelewa hili limewezekanaje.
Petro Azungumza na Watu
11 Huku wakishangaa, watu wale waliwakimbilia Petro na Yohana pale walikokuwa katika Ukumbi wa Sulemani. Mtu yule aliyeponywa alikuwa akingali amewang'anga'nia Petro na Yohana.
12 Petro alipoona hili, aliwaambia watu: “Ndugu zangu Wayahudi, kwa nini mnashangaa hili? Mnatutazama kama vile ni kwa nguvu zetu tumemfanya mtu huyu atembee. Mnadhani hili limetendeka kwa sababu sisi ni wema? 13 Hapana, Mungu ndiye aliyetenda hili! Ni Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo. Ni Mungu aliyeabudiwa na baba zetu wote. Kwa kufanya hili, alimtukuza Yesu mtumishi wake, yule ambaye ninyi mlimtoa ili auawe. Pilato alipotaka kumwachia huru, mlimwambia Pilato kuwa hamumtaki Yesu. 14 Yesu alikuwa Mtakatifu na mwema, lakini mlimkataa na badala yake mlimwambia Pilato amwache huru mwuaji[a] na awape ninyi. 15 Na hivyo mlimwua yule awapaye uzima! Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu. Sisi ni mashahidi wa jambo hili kwani tuliliona kwa macho yetu wenyewe.
16 Huyu mlemavu wa miguu ameponywa kwa sababu tunalo tumaini katika Yesu. Nguvu ya Yesu ndiyo iliyomponya. Mnamwona na mnamfahamu mtu huyu. Ameponywa kabisa kwa sababu ya imani inayotokana na Yesu. Ninyi nyote mmeona hili likitokea!
17 Kaka zangu, ninajua kwamba hamkujua mlilomtendea Yesu wakati ule. Hata viongozi wenu hawakujua walilokuwa wanatenda. 18 Lakini Mungu alikwishasema kupitia manabii kuwa mambo haya yangetokea. Masihi wake angeteseka na kufa. Nimewaambia jinsi ambavyo Mungu alifanya jambo hili likatokea. 19 Hivyo lazima mbadili mioyo na maisha yenu. Mrudieni Mungu, naye atawasamehe dhambi zenu. 20 Kisha Bwana atawapa muda wa faraja kutokana na masumbufu yenu. Atamtuma Yesu kwenu, aliyemchagua kuwa Masihi wenu.
21 Lakini Yesu lazima akae mbinguni mpaka wakati ambapo kila kitu kitafanywa upya tena. Mungu alikwisha sema kuhusu wakati huu tangu zamani kupitia manabii wake watakatifu. 22 Musa alisema, ‘Bwana Mungu wako atakupa nabii. Nabii huyo atatoka miongoni mwa watu wako. Atakuwa kama mimi. Ni lazima mtii kila kitu atakachowaambia. 23 Na yeyote atakayekataa kumtii nabii huyo atakufa na kutengwa na watu wa Mungu.’(A)
24 Samweli, na manabii wengine wote walisema kwa niaba ya Mungu. Baada ya Samweli, walisema kuwa wakati huu ungekuja. 25 Na kile ambacho manabii walikisema ni kwa ajili yenu ninyi wazaliwa wao. Mmepokea Agano ambalo Mungu alilifanya na baba zenu. Mungu alimwambia baba yenu Ibrahimu kuwa, ‘Kila taifa duniani litabarikiwa kupitia wazaliwa wako.’(B) 26 Mungu amemtuma Yesu, mtumishi wake maalumu. Alimtuma kwenu kwanza, ili awabariki kwa kuwageuza kila mmoja wenu aache njia zake za uovu.”
Footnotes
- 3:14 mwuaji Baraba, mtu ambaye Wayahudi walichagua aachiwe huru badala ya Yesu. Tazama Lk 23:18.
Copyright © 2017 by Bible League International