Add parallel Print Page Options

Paulo Azungumza Mbele za Watu

22 Paulo akasema, “Baba zangu na kaka zangu, nisikilizeni! Nitajitetea kwenu.”

Wayahudi walipomsikia Paulo anazungumza kwa Kiaramu wakanyamaza. Kisha Paulo akasema,

“Mimi ni Myahudi, nilizaliwa katika mji wa Tarso katika jimbo la Kilikia. Nilikulia hapa katika mji huu. Nilikuwa mwanafunzi wa Gamalieli[a] ambaye kwa umakini alinifundisha kila kitu kuhusu sheria ya baba zetu. Daima nimekuwa na shauku ya kumheshimu Mungu, sawa na ninyi nyote hapa leo. Niliwatesa watu walioifuata Njia. Baadhi yao hapa waliuawa kwa sababu yangu. Niliwakamata wanaume na wanawake na kuwaweka gerezani.

Kuhani mkuu na baraza lote la wazee wa Wayahudi wanaweza kuwathibitishia hili. Wakati mmoja viongozi hawa walinipa barua. Barua hizo waliandikiwa ndugu zetu Wayahudi katika mji wa Dameski. Nilikuwa naenda huko kuwakamata wafuasi wa Yesu na kuwaleta Yerusalemu ili waadhibiwe.

Paulo Aeleza Kuhusu Kuokolewa Kwake

Lakini kitu fulani kilinitokea nikiwa njiani kwenda Dameski. Ilipokuwa inakaribia mchana na nilikuwa karibu na mji wa Dameski. Ghafla mwanga kutoka mbinguni ulining'aria kunizunguka. Nilianguka chini na nikasikia sauti ikiniambia, ‘Sauli, Sauli kwa nini unanitesa?’

Niliuliza, ‘Wewe ni nani, Bwana?’ Sauti ikasema, ‘Mimi ni Yesu kutoka Nazareti, unayemtesa.’ Watu waliokuwa pamoja nami hawakuisikia sauti lakini waliona mwanga.

10 Nilisema, ‘Nifanye nini Bwana?’ Bwana alinijibu, ‘Simama na uingie Dameski. Humo utawaambia yote niliyopanga uyafanye.’ 11 Sikuweza kuona kwa sababu mwanga ule angavu ulinilemaza macho. Hivyo wale watu waliokuwa pamoja nami waliniongoza kuingia mjini Dameski.

12 Alikuwepo mtu mmoja katika mji wa Dameski aliyeitwa Anania.[b] Mtu huyu alikuwa mcha Mungu na aliitii Sheria ya Musa na Wayahudi wote walioishi kule walimheshimu. 13 Alikuja kwangu na kuniambia, ‘Sauli, ndugu yangu, tazama juu na uone tena!’ Ghafla niliweza kumwona.

14 Anania aliniambia, ‘Mungu yule yule aliyeabudiwa na baba zetu alikuchagua wewe tangu zamani kuujua mpango wake. Amekuchagua wewe kumwona Mwenye Haki wake na kusikia maneno kutoka kwake. 15 Utakuwa shahidi wake kwa watu wote. Utawaambia ulichoona na kusikia. 16 Sasa usisubiri zaidi. Simama, ubatizwe na usafishwe dhambi zako, mwamini Yesu ili akuokoe.’[c]

17 Baadaye, nilirudi Yerusalemu. Nilipokuwa naomba katika eneo la hekalu, nikaona maono. 18 Nilimwona Yesu, naye akaniambia, ‘Haraka, ondoka Yerusalemu sasa hivi! Watu hapa hawataukubali ukweli unaowaambia kuhusu mimi.’

19 Nilisema, ‘Lakini, Bwana, Wayahudi wanajua kuwa mimi ndiye niliyewafunga gerezani na kuwapiga wale wanaokuamini wewe. Nilikwenda kwenye masinagogi yote kuwatafuta na kuwakamata Wayahudi wanaokuamini wewe. 20 Watu wanajua pia kuwa nilikuwepo wakati Stefano shahidi wako, alipouawa. Nilisimama pale na kukubaliana nao kuwa wamwue. Nilishikilia hata mavazi ya watu waliokuwa wanamwua!’

21 Lakini Yesu akaniambia, ‘Ondoka sasa. Nitakutuma mbali sana kwa watu wasio Wayahudi.’”

22 Watu waliacha kusikiliza Paulo aliposema jambo hili la mwisho. Walipasa sauti wote, wakisema, “Mwondosheni mtu huyu! Hastahili kuishi katika dunia hii tena.” 23 Waliendelea kupiga kelele, wakichana nguo zao na kurusha mavumbi juu.[d] 24 Ndipo kamanda akawaambia askari wamwingize Paulo kwenye jengo la jeshi na wampige. Alitaka kumlazimisha Paulo aeleze ni kwa nini watu walikuwa wanampigia kelele namna ile. 25 Askari walipokuwa wanamfunga Paulo, wakijiandaa kumpiga alimwuliza ofisa wa jeshi, “Je, mna haki ya kumpiga raia wa Rumi[e] ambaye hajathibitika kuwa na hatia?”

26 Ofisa aliposikia hili, alikwenda kwa kamanda na kumwambia. Ofisa alisema, “Unafahamu unalolifanya? Mtu huyu ni raia wa Rumi!”

27 Kamanda akaenda kwa Paulo na kusema, “Niambie kwa hakika, ‘Je, wewe ni raia wa Rumi?’”

Paulo akajibu, “Ndiyo.”

28 Kamanda akasema, “Nililipa pesa nyingi kuwa raia wa Rumi.”

Lakini Paulo akasema, “Nilizaliwa raia wa Rumi.”

29 Ghafla watu waliokuwa wanajiandaa kumwuliza maswali Paulo waliondoka. Kamanda aliogopa kwa sababu alikuwa ameshamfunga Paulo kwa minyororo na ni raia wa Rumi.

Paulo Aongea na Viongozi wa Kiyahudi

30 Siku iliyofuata kamanda alitaka kujua ni kwa nini Wayahudi wanamshitaki Paulo. Hivyo aliamuru viongozi wa makuhani na baraza kuu lote kukutana pamoja. Alimfungua Paulo minyororo na kumleta mbele ya baraza.

Footnotes

  1. 22:3 Gamalieli Alikuwa mwalimu muhimu sana wa Mafarisayo, Kikundi cha kidini cha Wayahudi. Tazama Mdo 5:34.
  2. 22:12 Anania Katika Matendo ya Mitume wapo watu watatu waliotumia jina hili. Tazama Mdo 5:1 na 23:2 kwa ajili ya wale wengine wawili.
  3. 22:16 mwamini Yesu ili akuokoe Kwa maana ya kawaida, “kuliitia jina lake”, kuonesha imani katika Yesu kwa kumwabudu au kumwomba kwa ajili ya msaada.
  4. 22:23 wakichana … mavumbi juu Matendo haya yalikuwa ishara ya hasira kali sana.
  5. 22:25 raia wa Rumi Sheria Rumi ilisema kwamba raia wa Rumi hawezi kuadhibiwa kabla ya kushitakiwa na kuhukumiwa baada ya kukutwa na hatia. Tazama pia Mdo 23:27.