Add parallel Print Page Options

Petro Arudi Yerusalemu

11 Mitume na waamini katika Uyahudi walisikia kwamba watu wasio Wayahudi wameyapokea mafundisho ya Mungu pia. Lakini Petro alipokuja Yerusalemu, baadhi ya waamini wa Kiyahudi[a] walimkosoa. Walisema, “Uliingia katika nyumba za watu wasio Wayahudi ambao hawajatahiriwa na ukala pamoja nao!”

Hivyo Petro akawaelezea namna ilivyotokea. Akasema, “Nilikuwa katika mji wa Yafa. Nilipokuwa nikiomba, niliona maono. Niliona kitu kikishuka chini kutoka mbinguni. Kilionekana kama shuka kubwa ikishushwa chini kwa pembe zake nne. Kikaja chini karibu yangu. Nilipotazama ndani yake, niliona aina zote za wanyama, pamoja na wale wa porini, wanyama wanaotambaa na ndege. Nilisikia sauti ikiniambia. Chinja chochote hapa na ule!”

“Lakini nilisema, ‘Siwezi kufanya hivyo Bwana! Sijawahi kula kitu cho chote kisicho safi au kisichostahili kuliwa kama chakula.’

Lakini sauti kutoka mbinguni ikajibu tena, ‘Mungu amevitakasa vitu hivi. Usiseme havistahili kuliwa!’

10 Hili lilitokea mara tatu. Ndipo kitu chote kikachukuliwa kurudi mbinguni. 11 Saa hiyo hiyo baada ya hayo wakawepo watu watatu wamesimama nje ya nyumba nilimokuwa ninakaa. Walikuwa wametumwa kutoka Kaisaria kunichukua. 12 Roho Mtakatifu aliniambia niende nao bila kuwa na mashaka. Ndugu hawa hapa sita walikwenda pamoja nami, na tulikwenda katika nyumba ya Kornelio. 13 Alitwambia kuhusu malaika aliyemwona amesimama katika nyumba yake. Malaika alimwambia, ‘Tuma baadhi ya watu waenda Yafa kumchukua Simoni, ambaye pia anaitwa Petro. 14 Atazungumza na wewe. Ujumbe atakaokwambia utakuokoa wewe na kila mtu anayeishi katika nyumba yako.’

15 Nilipoanza kuzungumza, Roho Mtakatifu alikuja juu yao kama vile alivyokuja juu yetu mwanzo.[b] 16 Ndipo nilikumbuka maneno ya Bwana Yesu, aliyosema: ‘Yohana alibatiza katika maji, lakini ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu.’ 17 Mungu amewapa watu hawa karama ile ile aliyotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo. Hivyo ningewezaje kupinga yale ambayo Mungu alitaka kufanya?”

18 Waamini wa Kiyahudi waliposikia hili, wakaacha kubisha. Wakamsifu Mungu na kusema, “Kwa hiyo Mungu anawaruhusu watu wasio Wayahudi kubadili mioyo yao na kuwa na maisha anayotoa!”

Habari Njema Zafika Antiokia

19 Waamini walitawanyika kwa sababu ya mateso[c] yaliyoanza baada ya Stefano kuuawa. Baadhi ya waamini walikwenda mbali mpaka Foeniki, Kipro na Antiokia. Walihubiri Habari Njema katika maeneo haya, lakini kwa Wayahudi tu. 20 Baadhi ya waamini hawa walikuwa watu kutoka Kipro na Kirene. Watu hawa walipofika Antiokia, walianza kuwahubiri watu wasio Wayahudi.[d] Waliwahubiri Habari Njema kuhusu Bwana Yesu. 21 Nguvu ya Bwana iliambatana na watu hawa, na idadi kubwa ya watu waliamini na kuamua kumfuata Bwana.

22 Kanisa katika mji wa Yerusalemu liliposikia kuhusu hili, lilimtuma Barnaba kwenda Antiokia. 23-24 Barnaba alikuwa mtu mwema, aliyejaa Roho Mtakatifu na imani. Alipokwenda Antiokia na kuona jinsi Mungu alivyowabariki waamini pale, alifurahi sana. Akawatia moyo wote, akasema, “Iweni waaminifu kwa Bwana daima. Mtumikieni Yeye kwa mioyo yenu yote.” Watu wengi zaidi wakawa wafuasi wa Bwana.

25 Kisha Barnaba alikwenda katika mji wa Tarso kumtafuta Sauli. 26 Alipompata, alimpeleka Antiokia. Walikaa pale mwaka mzima. Kila wakati kanisa lilipokusanyika, Barnaba na Sauli walikutana nao na kuwafundisha watu wengi. Ni katika mji wa Antiokia ambako wafuasi wa Bwana Yesu walianza kuitwa “Wafuasi wa Kristo”.[e]

27 Katika wakati huo huo baadhi ya manabii walitoka Yerusalemu na kwenda Antiokia. 28 Mmoja wao, aliyeitwa Agabo, huku akisaidiwa na Roho Mtakatifu, alisimama na kuzungumza. Alisema, “Wakati mbaya sana unakuja katika dunia yote. Hakutakuwa chakula kwa ajili ya watu kula.” (Kipindi hiki cha njaa kilitokea Klaudio alipokuwa mtawala wa Kirumi) 29 Wafuasi wa Bwana wakaamua kwamba kila mmoja wao atatuma kiasi anachoweza kuwasaidia ndugu wote[f] wanaoishi Uyahudi. 30 Walikusanya pesa na kuwapa Barnaba na Sauli, waliozipeleka kwa wazee, katika Uyahudi.

Footnotes

  1. 11:2 waamini wa Kiyahudi Kwa maana ya kawaida, “watu wa tohara”. Hii inaweza kuwa na maana ya Wayahudi waliodhani kuwa wafuasi wote wa Kristo ni lazima watahiriwe na kutii Sheria ya Musa. Tazama Gal 2:12.
  2. 11:15 mwanzo Siku ya Pentekoste katika Matendo 2, Roho Mtakatifu alipowashukia wafuasi wa mwanzo wa Yesu na kuwapa nguvu ya kuanza kuuhubiri ulimwengu Habari Njema za wokovu kupitia Yesu.
  3. 11:19 mateso Au “kipindi cha mateso”. Hiki ni kipindi ambacho viongozi wa Kiyahudi katika mji wa Yerusalemu walikuwa wakiwaadhibu watu wanaomwamini Kristo. Tazama Mdo 8:1-4.
  4. 11:20 watu wasio Wayahudi Kwa maana ya kawaida, “Wa mataifa” au “Wahelenisti”, au watu waliochangamana na kuathiriwa na utamaduni wa Kiyunani (Kigiriki). Nakala zingine za Kiyunani zina “Wayunani” au “Wagiriki”.
  5. 11:26 Wafuasi wa Kristo Yaani, Wakristo.
  6. 11:29 ndugu wote Yaani, Jamaa yote ya Waamini.