Add parallel Print Page Options

Luka Aandika Kitabu Kingine

Mpendwa Theofilo:

Katika kitabu cha kwanza niliandika kuhusu kila kitu ambacho Yesu alitenda na kufundisha tangu mwanzo mpaka siku alipochukuliwa juu mbinguni. Kabla hajaondoka, alizungumza na mitume aliowachagua kwa msaada wa Roho Mtakatifu kuhusu mambo waliyotakiwa kufanya. Hii ilikuwa baada ya kifo chake, ambapo aliwathibitishia kwa namna nyingi kuwa alikuwa hai. Mitume walimwona Yesu mara nyingi kwa muda wa siku arobaini baada ya kufufuka kutoka kwa wafu. Naye Yesu alizungumza nao kuhusu ufalme wa Mungu. Wakati mmoja Yesu alipokuwa akila pamoja nao, aliwaambia wasiondoke Yerusalemu. Aliwaambia, “Kaeni hapa mpaka mtakapopokea kile ambacho Baba aliahidi kutuma. Kumbukeni, niliwaambia juu yake. Yohana aliwabatiza watu kwa maji, lakini baada ya siku chache mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.”

Yesu Achukuliwa Juu Mbinguni

Mitume walipokuwa pamoja, walimwuliza Yesu, “Bwana, huu ni wakati wako wa kuwarudishia Waisraeli ufalme wao tena?”

Yesu akawaambia, “Baba peke yake ndiye mwenye mamlaka ya kuamua tarehe na nyakati. Si juu yenu kujua. Lakini Roho Mtakatifu atawajia na kuwapa nguvu. Nanyi mtakuwa mashahidi wangu. Mtawahubiri watu kuhusu mimi kila mahali, kuanzia humu Yerusalemu, Uyahudi yote, katika Samaria na hatimaye kila mahali ulimwenguni.”

Baada ya kusema haya, alichukuliwa juu mbinguni. Walipokuwa wanaangalia juu angani, wingu lilimficha na hawakuweza kumwona. 10 Walikuwa bado wanatazama angani alipokuwa anakwenda. Ghafla malaika wawili waliovaa mavazi meupe wakasimama pembeni mwao. 11 Wakasema, “Enyi watu wa Galilaya, kwa nini mmesimama hapa na mnatazama angani? Mlimwona Yesu akichukuliwa kutoka kwenu kwenda mbinguni. Atarudi katika namna hii hii kama mlivyomwona akienda.”

Mtume Mpya Achaguliwa

12 Ndipo mitume walirudi Yerusalemu kutoka Mlima wa Mizeituni, ulio umbali wa kama kilomita moja[a] kutoka Yerusalemu. 13 Walipoingia mjini, walikwenda kwenye chumba cha ghorofani walikokuwa wanakaa. Hawa ndiyo wale waliokuwepo: Petro, Yohana, Yakobo, na Andrea, Filipo, Thomasi, Bartholomayo, Mathayo, Yakobo (mwana wa Alfayo), na Simoni Mzelote, na Yuda (mwana wa Yakobo).

14 Mitume hawa wote walikuwa pamoja na waliomba kwa nia moja. Baadhi ya wanawake, Mariamu mama wa Yesu na wadogo zake Bwana Yesu walikuwepo pale pamoja na mitume.

15 Baada ya siku chache waamini waliokuwa kama mia moja na ishirini walikutana pamoja. Petro alisimama na kusema, 16-17 “Kaka na dada zangu, katika Maandiko Roho Mtakatifu alisema kupitia Daudi kwamba jambo fulani lazima litatokea. Alizungumza kuhusu Yuda, yule aliyekuwa katika kundi letu wenyewe. Yuda alihudumu pamoja nasi. Roho alisema Yuda atawaongoza watu kumkamata Yesu.”

18 (Kwa kufanya hili Yuda alilipwa pesa. Alinunulia shamba pesa hizo. Lakini aliangukia kichwa chake, mwili wake ukapasuka, na matumbo yake yote yakamwagika nje. 19 Na watu wote wa Yerusalemu wanalijua hili. Ndiyo maana waliliita shamba hilo Akeldama, ambalo maana yake kwa Kiaramu ni “Shamba la Damu”.)

20 Petro akasema, “Katika kitabu cha Zaburi, jambo hili limeandikwa kuhusu Yuda:

‘Watu wasipakaribie mahali pake;
    Yeyote asiishi hapo.’(A)

Pia imeandikwa kuwa:

‘Mtu mwingine achukue kazi yake.’(B)

21-22 Hivyo ni lazima mtu mwingine ajiunge nasi ili awe shahidi wa ufufuo wa Bwana Yesu. Ni lazima awe mmoja wa wale waliokuwa katika kundi letu wakati wote Bwana Yesu alipokuwa pamoja nasi. Ni lazima awe yule ambaye amekuwa pamoja nasi tangu Yohana alipokuwa anabatiza watu mpaka siku ambayo Bwana Yesu alichukuliwa kutoka kwetu na kwenda mbinguni.”

23 Kisha waliwasimamisha watu wawili mbele ya kundi. Mmoja aliitwa Yusufu Barsaba, ambaye pia aliitwa Yusto. Mwingine aliitwa Mathiasi. 24-25 Wakaomba wakisema, “Bwana unajua mioyo ya watu wote. Tuonyeshe kati ya watu hawa wawili uliyemchagua kufanya kazi hii. Yuda aliiacha na kuifuata njia yake. Bwana tuonyeshe ni nani achukue sehemu yake kama mtume!” 26 Kisha wakapiga kura kumchagua mmoja kati ya watu hao wawili. Kura ikaonesha Mathiasi ndiye Bwana anamtaka. Hivyo akawa mtume pamoja na wale wengine kumi na moja.

Footnotes

  1. 1:12 kilomita moja Ama mwendo wa Sabato, ambao ni sawa na umbali wa kilomita moja: Waisraeli hawakuruhusiwa kusafiri zaidi ya futi 3,600 (kati ya yadi 1,000-1,200) siku ya Sabato. Umbali huu ulitokana na umbali kati ya sanduku la Agano na watu waliokuwa wakilifuata (tazama Yos 3:4). Pia ilichukuliwa kuwa ni umbali ambao mtu alitakiwa kuwalisha wanyama wake (Hes 35:4,5).