Add parallel Print Page Options

Yesu Amweka Huru Mtu Kutoka Pepo Wachafu

(Mt 8:28-34; Lk 8:26-39)

Wakafika ng'ambo ya ziwa, katika nchi walimoishi Wagerasi.[a] Yesu alipotoka katika mashua ile ghafla, mtu mmoja aliyekuwa na roho chafu alitoka makaburini kuja kumlaki. Mtu huyu aliishi makaburini, na hakuna mtu yeyote aliyeweza kumfunga hata kwa mnyororo, Watu walijaribu kila mara kumfunga kwa minyororo na vyuma kwenye miguu na mikono. Hata hivyo, aliweza kuivunja minyororo ile na pingu zile za vyuma wala hakuna aliyekuwa na nguvu za kutosha kumdhibiti. Kila mara usiku na mchana akiwa makaburini na kwenye milima alipiga kelele na kujikata kwa mawe.

Alipomwona Yesu kutoka mbali, alimkimbilia, na kusujudu mbele yake. Kisha akalia kwa sauti kubwa na kusema, “Unataka nini kwangu, Yesu Mwana wa Mungu Aliye Mkuu zaidi? Nakuomba uape mbele za Mungu kwamba hutanitesa.” Yule pepo alisema haya kwa sababu Yesu alikuwa anamwambia, “Mtoke huyo mtu, ewe pepo mchafu!”

Ndipo Yesu akamwuliza yule mtu, “Jina lako nani?”

Naye akamjibu, “Jina langu ni Jeshi,[b] kwa sababu tuko wengi.” 10 Yule pepo akamwomba Yesu tena na tena asiwaamuru kutoka katika eneo lile.

11 Kulikuwepo kundi kubwa la nguruwe likila katika kilima. 12 Wale pepo wakamwomba Yesu awatume waende katika lile kundi la nguruwe na kuliingia, 13 Naye akawaruhusu. Kwa hiyo pepo wachafu walimtoka mtu yule na kuwaingia nguruwe.[c] Kundi lile lilikuwa na idadi karibu ya elfu mbili, lilikimbia kuelekea kwenye kingo zenye mtelemko mkali na kutumbukia ziwani, ambamo walizama.

14 Wale waliowachunga walikimbia. Wakatoa taarifa mjini na katika maeneo jirani ya mashambani. Watu wakaja kuona ni kitu gani kilichotokea. 15 Watu hao wakamwendea Yesu. Nao wakamwona yule aliyekuwa na mashetani ameketi mahali pale, amevaa nguo na akiwa mwenye akili zake nzuri; huyu ni yule aliyekuwa amepagawa na jeshi la mashetani. Wakaogopa. 16 Wale waliokuwa wameona hili waliwasimulia kile kilichomtokea mtu yule aliyekuwa amepagawa na mashetani na kuhusu nguruwe wale. 17 Nao wakamwomba Yesu aondoke katika eneo lile.

18 Wakati Yesu akipanda katika mtumbwi, mtu yule aliyekuwa amepagawa na mashetani alimwomba Yesu afuatane naye. 19 Lakini Yesu hakumruhusu aende naye, isipokuwa alimwambia, “Nenda kwa watu wa kwenu, na uwaambie yote ambayo Bwana amekufanyia, na uwaambie jinsi alivyokuwa na huruma kwako.”

20 Hivyo mtu yule aliondoka, na akaanza kuwaeleza watu katika Dekapoli[d] mambo mengi ambayo Yesu amemtendea, na watu wote walistaajabu.

Read full chapter

Footnotes

  1. 5:1 Wagerasi Nakala zingine za Kiyunani zina “Wagadarini” na zingine zimewaita “Wagergesini”.
  2. 5:9 Jeshi Jina hili lina maana nyingi sana. Jina hili lina maana “wengi zaidi” Ni neno lililotumika kwa kundi la wanajeshi 6,000 wa Jeshi la Kirumi.
  3. 5:13 nguruwe Watu kijijini walikuwa wakiwatunza nguruwe katika kundi moja kubwa. Kundi hilo lilikuwa chanzo muhimu cha mapato kwa kijiji.
  4. 5:20 Dekapoli Eneo wanaloishi wasio Wayahudi mashariki mwa Galilaya inaloitwa pia Eneo la Miji Kumi.