Marko 3:1-6
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Yesu Amponya Mtu Siku ya Sabato
(Mt 12:9-14; Lk 6:6-11)
3 Kwa mara nyingine tena Yesu alikwenda kwenye sinagogi. Huko alikuwepo mtu aliyekuwa na mkono uliolemaa. 2 Watu wengine walikuwa wakimwangalia Yesu kwa karibu sana. Walitaka kuona ikiwa angemponya mtu yule siku ya Sabato,[a] ili wapate sababu ya kumshitaki. 3 Yesu akamwambia yule mtu aliyekuwa na mkono uliolemaa, “Simama mbele ili kila mtu akuone.”
4 Ndipo Yesu akawaambia, “Je, ni halali kutenda mema ama kutenda mabaya siku ya Sabato? Je, ni halali kuyaokoa maisha ya mtu fulani ama kuyapoteza?” Lakini wao walikaa kimya.
5 Yesu akawatazama wote waliomzunguka kwa hasira lakini alihuzunika kwa sababu waliifanya mioyo yao kuwa migumu. Akamwambia mtu yule “nyosha mkono wako”, naye akaunyosha, na mkono wake ukapona. 6 Kisha Mafarisayo wakaondoka na papo hapo wakaanza kupanga njama pamoja na Maherode kinyume cha Yesu kutafuta jinsi gani wanaweza kumuua.
Read full chapterFootnotes
- 3:2 Walitaka … siku ya Sabato Haikuruhusiwa kwa Wayahudi kufanya kazi siku ya Sabato na wengi waliamini kumponya mtu ambaye hakuwa katika hatari ya kufa ilikuwa ni kazi.
Copyright © 2017 by Bible League International