Add parallel Print Page Options

Yesu Achagua Baadhi ya Wafuasi

(Mt 4:18-22; Mk 1:16-20)

Yesu aliposimama ukingoni mwa Ziwa Galilaya[a] kundi la watu lilimsogelea ili wasikie mafundisho kuhusu Mungu. Yesu aliona mashua mbili zikiwa kando ya ziwa. Wavuvi walikuwa wametoka katika mashua zao na walikuwa wanaosha nyavu zao. Yesu aliingia kwenye mashua ya Simoni. Akamwomba Simoni aisogeze mbali kidogo na ufukwe wa ziwa. Kisha akaketi ndani ya mashua na akawafundisha watu waliokuwa ufukweni mwa ziwa.

Yesu alipomaliza kufundisha, alimwambia Simoni, “Ipeleke mashua mpaka kwenye kilindi cha maji kisha mshushe nyavu zenu majini na mtapata samaki.”

Simoni akamjibu, “Bwana, tumejitahidi usiku kucha kuvua samaki na hatukupata chochote. Lakini kwa kuwa unasema nishushe nyavu majini, nitafanya hivyo.” Walipofanya hivi, nyavu zao zilijaa samaki wengi mpaka zikaanza kuchanika. Waliwaita rafiki zao waliokuwa katika mashua nyingine ili waje wawasaidie. Rafiki zao walikuja kuwasaidia, na mashua zote mbili zilijaa samaki kiasi cha kutaka kuzama.

8-9 Wavuvi wote walistaajabu kwa sababu ya wingi wa samaki waliovua. Simoni Petro alipoona hili, akapiga magoti mbele ya Yesu na akasema, “Nenda mbali nami Bwana, mimi ni mwenye dhambi!” 10 Yakobo na Yohana wana wa Zebedayo, walishangaa pia. (Yakobo na Yohana walikuwa wanavua pamoja na Simoni.)

Yesu akamwambia Simoni, “Usiogope. Kuanzia sasa kazi yako haitakuwa kuvua samaki bali kukusanya watu!”

11 Wakaziendesha mashua zao mpaka pwani, kisha wakaacha kila kitu na kumfuata Yesu.

Yesu Amponya Mgonjwa

(Mt 8:1-4; Mk 1:40-45)

12 Wakati mmoja Yesu alikuwa katika mji ambao mwanaume mmoja mgonjwa alikuwa anaishi. Mwanaume huyo alikuwa na ugonjwa mbaya sana wa ngozi mwili wake wote. Alipomwona Yesu, alimsujudia na kumsihi akisema, “Bwana, ikiwa unataka una uwezo wa kuniponya.”

13 Yesu akasema, “Hakika ninataka kukuponya, upone!” Kisha akamgusa, na ugonjwa ukatoweka papo hapo. 14 Yesu akamwambia, “Usimwambie mtu yeyote kilichotokea. Lakini nenda kwa kuhani akakuchunguze.[b] Na umtolee Mungu sadaka ambazo Musa aliamuru watu wanaoponywa watoe, ili iwe ushahidi kwa watu kwamba umepona.”

15 Lakini habari kuhusu Yesu zilizidi kuenea zaidi. Watu wengi walikuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao. 16 Mara nyingi Yesu alikwenda sehemu zingine zisizokuwa na watu na akaomba huko.

Yesu Amponya Aliyepooza

(Mt 9:1-8; Mk 2:1-12)

17 Siku moja Yesu alikuwa anawafundisha watu. Mafarisayo na walimu wa sheria walikuwa wameketi hapo pia. Walitoka katika kila mji wa Galilaya, na Uyahudi, na Yerusalemu. BWANA alimpa Yesu uwezo wa kuponya watu. 18 Alikuwepo mtu aliyepooza na baadhi ya watu walikuwa wamembeba kwenye machela. Walijaribu kumwingiza ndani ili wamweke mbele ya Yesu. 19 Lakini walishindwa kufika alipokuwa Yesu kwa sababu kulikuwa na watu wengi sana. Hivyo walikwenda juu ya paa ya nyumba na kumshusha aliyepooza chini kupitia tundu kwenye dari. Waliishusha machela alimokuwa aliyepooza kwa usawa kiasi kwamba akawa amelala mbele ya Yesu. 20 Yesu alipoona imani waliyokuwa nayo, akamwambia yule mgonjwa: “Rafiki yangu, dhambi zako zimesamehewa!”

21 Walimu wa sheria na Mafarisayo wakaanza kuhojiana wao kwa wao wakisema: “Huyu mtu ni nani kiasi cha kuthubutu kusema hivi? Si anamtukana Mungu! Mungu peke yake ndiye anayesamehe dhambi.”

22 Lakini Yesu alijua walichokuwa wanawaza, akawaambia: “Kwa nini mna maswali haya mioyoni mwenu? 23-24 Wakati akiwa duniani Mwana wa Adamu anayo mamlaka ya kusamehe dhambi. Lakini nitawezaje kulithibitisha hili kwenu? Pengine mnafikiri ilikuwa rahisi kwangu kumwambia mtu huyu aliyepooza, ‘Dhambi zako zimesamehewa.’ Kwa sababu hilo haliwezi kuthibitishwa kwamba hakika limetokea. Lakini vipi nikimwambia, mtu huyu, beba machela yako na utembee? Hapo ndipo mtakapoweza kuona kama kweli ninayo mamlaka hayo ama sina.” Kwa hiyo Yesu akamwambia mtu yule aliyepooza, “Nitalithibitishaje hili kwako? Ninakwambia hivi, Inuka! Beba machela yako uende nyumbani!”

25 Yule mtu akasimama saa ile ile mbele ya kila mtu. Akaubeba machela yake na kwenda nyumbani kwake, akimsifu Mungu. 26 Kila mtu alishangaa na kuanza kumsifu Mungu. Wakajawa na hofu kuu baada ya kuiona nguvu ya Mungu. Wakasema, “Leo tumeona mambo ya kushangaza!”

Lawi (Mathayo) Amfuata Yesu

(Mt 9:9-13; Mk 2:13-17)

27 Baada ya hayo Yesu alitoka nje akamwona mtoza ushuru amekaa sehemu yake ya kukusanyia ushuru. Jina lake aliitwa Lawi. Yesu akamwambia, “Nifuate!” 28 Lawi akasimama, akaacha kila kitu na kumfuata Yesu.

29 Lawi akaandaa chakula cha usiku nyumbani kwake kwa kumheshimu Yesu. Mezani walikuwepo watoza ushuru wengi na baadhi ya watu wengine. 30 Lakini Mafarisayo na wale wanaofundisha sheria kwa ajili ya Mafarisayo wakaanza kulalamika kwa wafuasi wa Yesu wakisema, “Kwa nini mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi wengine?”

31 Yesu akawajibu, “Wagonjwa ndiyo wanaohitaji daktari, si wenye afya njema. 32 Sikuja kuwaambia wenye haki wabadilike, bali wenye dhambi.”

Swali Kuhusu Kufunga

(Mt 9:14-17; Mk 2:18-22)

33 Baadhi ya watu wakamwambia Yesu, “Wafuasi wa Yohana hufunga na kuomba mara kwa mara, vivyo hivyo wafuasi wa Mafarisayo. Lakini wafuasi wako hula na kunywa kila wakati.”

34 Yesu akawaambia, “Kwenye harusi huwezi kuwaambia marafiki wa bwana harusi wafunge wakati bwana harusi bado yuko pamoja nao. 35 Lakini muda ukifika na bwana harusi akaondolewa kwao. Watakuwa na huzuni, na watafunga.”

36 Yesu akawaambia mfano huu: “Hakuna anayekata kiraka kwenye vazi jipya na kukishona kwenye vazi la zamani. Ataharibu vazi jipya, na kiraka kutoka vazi jipya hakitakuwa sawa na vazi la zamani. 37 Pia hakuna mtu anayeweka divai mpya[c] katika viriba vya zamani. Divai mpya itavipasua, divai itamwagika, na viriba vitaharibika. 38 Daima mnaweka divai mpya kwenye viriba vipya. 39 Hakuna mtu ambaye baada ya kunywa divai ya zamani hutaka divai mpya. Kwa sababu husema, ‘Divai ya zamani ni nzuri.’”

Footnotes

  1. 5:1 Galilaya Kwa maana ya kawaida, “Genesareti”.
  2. 5:14 kuhani akakuchunguze Sheria ya Musa ilisema ni lazima kuhani aamue ikiwa mtu aliyekuwa na ukoma amepona.
  3. 5:37 divai mpya Maji ya zabibu ambayo ndiyo yanaanza kuchachuka na hutengeneza mgandamizo ndani ya chombo kilichofungwa.