Luka 1
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Luka Aandika Kuhusu Maisha ya Yesu
1 Mheshimiwa Theofilo:[a]
Watu wengine wengi wamejaribu kuandika juu ya mambo yaliyotokea katikati yetu ili kuukamilisha mpango wa Mungu. 2 Mambo hayo waliyoyaandika yanalingana na yale tuliyosikia kutoka kwa watu walioyaona tangu mwanzo. Na walimtumikia Mungu kwa kuwaambia wengine ujumbe wake. 3 Nimechunguza kila kitu kwa makini tangu mwanzo. Na nimeona kuwa ni vyema nikuandikie kwa mpangilio mzuri. 4 Nimefanya hivi ili uwe na uhakika kuwa yale uliyofundishwa ni ya kweli.
Malaika Amjulisha Zakaria Kuhusu Kuzaliwa kwa Yohana Mbatizaji
5 Herode alipokuwa mfalme wa Uyahudi, alikuwepo kuhani mmoja aliyeitwa Zakaria, aliyekuwa mmoja wa makuhani wa kikundi[b] cha Abiya. Mkewe alikuwa mzaliwa wa ukoo wa Haruni, na jina lake alikuwa Elizabeti. 6 Wote wawili Zakaria na Elizabeti walikuwa wema waliompendeza Mungu na daima walifanya yote yaliyoamriwa na Bwana na kila mara walifuata maagizo yake kwa ukamilifu. 7 Lakini hawakuwa na watoto kwa sababu Elizabeti alikuwa tasa, na wote wawili walikuwa wazee sana.
8 Ilipofika zamu ya kundi la Zakaria kuhudumu Hekaluni, yeye mwenyewe alikuwepo ili kuhudumu kama kuhani mbele za Mungu kwa ajili kundi. 9 Makuhani walikuwa wanapiga kura kumchagua mmoja wao atakayeingia katika Hekalu la Bwana ili kufukiza uvumba. Na Zakaria alichaguliwa wakati huu. 10 Wakati wa kufukiza uvumba ulipofika watu wote walikusanyika nje ya Hekalu wakiomba.
11 Zakaria akiwa ndani ya Hekalu alitokewa na malaika wa Bwana akiwa amesimama mbele yake upande wa kulia wa madhabahu ya uvumba. 12 Zakaria alipomwona malaika aliogopa, na akaingiwa na hofu. 13 Lakini Malaika akamwambia, “Usiogope, Zakaria. Mungu amelisikia ombi lako. Mkeo Elizabeti atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utamwita jina lake Yohana. 14 Utafurahi sana, na watu wengine wengi watamfurahia pamoja nawe. 15 Atakuwa mkuu kwa ajili ya Bwana. Kamwe asinywe mvinyo wala kitu chochote kile kitakachomlewesha. Atajazwa Roho Mtakatifu tangu akiwa tumboni mwa mama yake.
16 Naye atawafanya Waisraeli wengi wamrudie Bwana Mungu wao. 17 Atamtangulia Bwana ili kuwaandaa watu kuupokea ujio wake. Atakuwa na nguvu na roho kama Eliya. Atawapatanisha wazazi na watoto wao na kuwafanya wale wasiomtii Mungu kubadilika na kuanza kumtii Mungu.”
18 Zakaria akamwambia malaika, “Nitajuaje kuwa haya unayosema ni ya kweli? Maana mimi ni mzee na mke wangu ana umri mkubwa pia.”
19 Malaika akamjibu, “Mimi ni Gabrieli, ambaye daima husimama mbele za Mungu nikiwa tayari. Amenituma kuzungumza nawe na kukujulisha habari hizi njema. 20 Sasa sikiliza! Hautaweza kuzungumza mpaka siku ambayo mambo haya yatatokea kwa sababu hukuyaamini yale niliyokwambia. Lakini nilichosema hakika kitatokea.”
21 Watu waliokuwa nje ya Hekalu wakimngojea Zakaria walishangaa kwa sababu alikaa kwa muda mrefu ndani ya Hekalu. 22 Zakaria alipotoka nje hakuweza kuzungumza nao. Aliwafanyia watu ishara kwa mikono yake. Hivyo watu walitambua kuwa alikuwa ameona maono alipokuwa Hekaluni. 23 Zamu ya utumishi wake ilipokwisha alirudi nyumbani.
24 Wakati fulani baadaye, Elizabeti, mke wa Zakaria akawa mjamzito. Alikaa katika nyumba yake na hakutoka nje kwa miezi mitano. Alisema, 25 “Na sasa, hatimaye Bwana amenisaidia kwa kuniondolea aibu yangu.”
Malaika Atangaza Kuzaliwa kwa Yesu
26-27 Mwezi wa sita wa ujauzito wa Elizabeti, Mungu alimtuma malaika Gabrieli kwa msichana mmoja bikira aliyeishi Nazareti, mji wa Galilaya. Msichana huyo alikuwa amechumbiwa na Yusufu mzaliwa katika ukoo wa Daudi. Jina la bikira huyo lilikuwa Mariamu. 28 Malaika alimwendea na kusema “Salamu! Bwana yu pamoja nawe; Kwa kuwa neema yake iko juu yako.”
29 Lakini, Mariamu alichanganyikiwa kutokana na yale aliyosema malaika. Akajiuliza, “Salamu hii ina maana gani?”
30 Malaika akamwambia, “Usiogope Mariamu, kwa kuwa neema ya Mungu iko juu yako. 31 Sikiliza! Utapata mimba na kuzaa mtoto mwanamume, nawe utamwita jina lake Yesu. 32 Mtoto huyo atakuwa Mkuu na watu watamwita Mwana wa Mungu Aliye Mkuu Sana na Bwana Mungu atamfanya kuwa mfalme kama Daudi baba yake. 33 Naye ataitawala nyumba ya Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho.”
34 Mariamu akamwambia malaika, “Jambo hili litatokeaje? Kwa maana mimi bado ni bikira.”
35 Malaika akamwambia Mariamu, “Roho Mtakatifu atakujia, na nguvu zake Mungu Mkuu zitakufunika. Na hivyo mtoto atakayezaliwa atakuwa mtakatifu na ataitwa Mwana wa Mungu. 36 Pia sikiliza hili: Jamaa yako Elizabeti ni mjamzito. Ijapokuwa ni mzee sana, atazaa mtoto wa kiume. Kila mtu alidhani hataweza kuzaa, lakini sasa huu ni mwezi wa sita wa ujauzito wake. 37 Mungu anaweza kufanya jambo lolote!”
38 Mariamu akasema, “Mimi ni mtumishi wa Bwana, basi jambo hili litokee kwangu kama ulivyosema.” Kisha malaika akaondoka.
Mariamu Amtembelea Elizabeti
39 Mariamu akajiandaa na kwenda haraka katika mji mmoja ulio vilimani katika jimbo la Yuda. 40 Alikwenda nyumbani kwa Zakaria, alipofika akamsalimu Elizabeti. 41 Elizabeti aliposikia salamu ya Mariamu, mtoto aliyekuwa tumboni mwake akirukaruka, na Elizabeti akajazwa Roho Mtakatifu.
42 Kisha akapaza sauti na kumwambia Mariamu, “Umebarikiwa kuliko wanawake wote, na mtoto utakayemzaa amebarikiwa. 43 Lakini jambo hili kuu limetokeaje kwangu, hata mama wa Bwana wangu aje kwangu? 44 Kwa maana sauti ya salamu yako ilipofika masikioni mwangu, mtoto aliye ndani yangu amerukaruka kwa furaha. 45 Umebarikiwa wewe uliyeamini kuwa mambo aliyokuambia Bwana yatatokea.”
Mariamu Amsifu Mungu
46 Mariamu akasema,
“Moyo wangu unamwadhimisha Bwana,
47 kwa maana, Yeye, Mungu na Mwokozi
wangu amenipa furaha kuu!
48 Kwa maana ameonesha kunijali,
mimi mtumishi wake, nisiye kitu.
Na kuanzia sasa watu wote
wataniita mbarikiwa.
49 Kwa kuwa Mwenye Nguvu amenitendea mambo makuu.
Jina lake ni takatifu.
50 Na huwapa rehema zake wale wamchao,
kutoka kizazi hadi kizazi.
51 Ameonesha nguvu ya mkono wake;
Amewatawanya wanaojikweza.
52 Amewaangusha watawala kutoka katika viti vyao vya enzi,
na kuwakweza wanyenyekevu.
53 Amewashibisha wenye njaa kwa mambo mema,
na amewatawanya matajiri bila ya kuwapa kitu.
54 Amemsaidia Israeli, watu aliowachagua ili wamtumikie.
Amekumbuka kuonesha rehema;
55 Maana ndivyo alivyowaahidi baba zetu,
Ibrahimu na wazaliwa wake.”
56 Mariamu alikaa na Elizabeti kwa muda wa kama miezi mitatu, kisha alirudi nyumbani kwake.
Kuzaliwa kwa Yohana Mbatizaji
57 Wakati ulipotimia kwa Elizabeti kujifungua, alizaa mtoto wa kiume. 58 Majirani na jamaa zake waliposikia jinsi Bwana alivyokuwa mwema kwake, walifurahi pamoja naye.
59 Mtoto alipofikisha umri wa siku nane, walikuja kumtahiri.[c] Walipotaka kumwita mtoto Zakaria kutokana na jina la baba yake. 60 Mama yake akasema, “Hapana, mtoto ataitwa Yohana.”
61 Lakini wao wakamwambia, “Hakuna jamaa yako hata mmoja mwenye jina hilo.” 62 Ndipo wakamfanyia ishara baba yake wakimwuliza jina alilotaka kumpa mtoto.
63 Zakaria akataka ubao wa kuandikia,[d] Kisha akaandika, “Jina lake ni Yohana.” Wote wakashangaa. 64 Mara hiyo hiyo mdomo wake ulifunguliwa na ulimi wake ukaachia, akaanza kuzungumza na kumsifu Mungu. 65 Majirani zao wakajawa hofu na watu katika sehemu zote za vilima katika jimbo la Yuda wakawa wanazungumza kuhusu jambo hili. 66 Watu wote waliosikia kuhusu mambo haya walijiuliza, wakisema, “Mtoto huyu atakuwa wa namna gani?” Kwa kuwa nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja naye.
Zakaria Amsifu Mungu
67 Kisha Zakaria, baba yake Yohana, akajaa Roho Mtakatifu, akatabiri, akisema:
68 “Asifiwe Bwana, Mungu wa Israeli,
kwa kuwa amekuja kuwasaidia
watu wake na kuwaweka huru.
69 Na ametuletea sisi Mwokozi Mwenye Nguvu,
kutoka katika ukoo wa mtumishi wake Daudi.
70 Hivi ndivyo alivyoahidi
kupitia manabii wake watakatifu tangu zamani.
71 Aliahidi kwa Agano kuwa atatuokoa na adui zetu
na milki za wote wanaotuchukia.
72 Ili kuonesha rehema kwa baba zetu,
na kulikumbuka agano lake takatifu aliloagana nao.
73 Agano hili ni kiapo alichomwapia
baba yetu Ibrahimu.
74 Alipoahidi kutuokoa kutoka katika nguvu za adui zetu,
ili tuweze kumwabudu Yeye bila hofu.
75 Katika namna iliyo takatifu na yenye haki
mbele zake siku zote za maisha yetu.
76 Sasa wewe, mtoto mdogo,
utaitwa nabii wa Mungu Aliye Juu Sana,
kwa sababu utamtangulia Bwana
kuandaa njia yake.
77 Utawaambia watu wake kwamba wataokolewa
kwa kusamehewa dhambi zao.
78 Kwa rehema ya upendo wa Mungu wetu,
siku mpya[e] itachomoza juu yetu kutoka mbinguni.
79 Kuwaangazia wale wanaoishi katika giza,
kwa hofu ya mauti,
na kuongoza hatua zetu
katika njia ya amani.”
80 Na hivyo mtoto Yohana akakua na kuwa na nguvu katika roho. Kisha akaishi maeneo yasiyo na watu mpaka wakati alipotokea hadharani akihubiri ujumbe wa Mungu kwa watu wa Israeli.
Footnotes
- 1:1 Theofilo Theofilo ndiye aliyemdhamini Luka katika mradi wa utafiti na uandishi wa kitabu hiki na kingine (Matendo ya Mitume). Ijapokuwa ni kama aliandikiwa yeye, makusudi ya mwandishi na Roho Mtakatifu ni kuwa watu wote wakisome. Theofilo maana yake ni “Mpendwa wa Mungu”.
- 1:5 makuhani wa kikundi Makuhani wa Kiyahudi waligawanywa katika vikundi 24. Tazama 1 Mambo ya Nyakati sura ya 24. Vikundi hivi 24 vya Makuhani vilihudumu katika Hekalu mjini Yerusalemu kwa zamu (mzunguko). Kila kikundi kilikuwa na zamu kwa wiki nzima, aghalabu wiki mbili kwa mwaka.
- 1:59 kumtahiri Yaani, kumfanyia tohara kama ilivyokuwa katika sheria ya Musa.
- 1:63 ubao wa kuandikia Ni ubao uliokuwa umepakwa nta au mpira ili usiloe.
- 1:78 siku mpya Kwa maana ya kawaida, “Alfajiri”, imetumika hapa kama ishara ikimaanisha Masihi, Bwana.
Copyright © 2017 by Bible League International