Add parallel Print Page Options

Msiwaruhusu Watu Wenu Waishi Katika Dhambi

Sitaki kuyaamini yale ninayosikia, ya kwamba kuna uzinzi katikati yenu. Na ni aina mbaya ya uzinzi ambayo hata wasiomwamini Mungu wetu hawauruhusu. Watu wanasema kuwa huko kwenu kuna mtu anayetenda dhambi ya zinaa na mke wa baba yake. Na mna kiburi! Mngepaswa kuwa na huzuni badala yake. Na mtu aliyetenda dhambi hiyo ilipaswa kuwa amefukuzwa kutoka katika kundi lenu. Siwezi kuwa hapo pamoja nanyi ana kwa ana, lakini niko pamoja nanyi katika roho. Na nimekwisha mhukumu mtu aliyetenda hii kama ambavyo ningemhukumu ikiwa ningekuwa hapo. Nanyi pia mnapaswa kufanya vivyo hivyo. Kusanyikeni pamoja katika jina la Bwana wetu Yesu. Nitakuwa pamoja nanyi katika roho, na nguvu ya Bwana Yesu itakuwa pamoja nanyi. Mtoeni mtu huyu kwa Shetani ili tabia yake ya kujisifu[a] iangamizwe lakini mtu mwenyewe na kanisa, lilojazwa Roho, liweze kuokolewa siku Bwana atakaporudi.

Kujisifu kwenu si kuzuri. Mnajua msemo unaosema, “Chachu kidogo huchahua donge zima.” Ondoeni chachu ya zamani ili muwe donge jipya. Ninyi kwa hakika ni mkate usio na chachu, mkate wa Pasaka,[b] Ndiyo, Kristo aliye Mwanakondoo wetu wa Pasaka[c] amekwisha usawa. Hivyo na tuule mlo wetu wa Pasaka, lakini si pamoja na mkate wenye chachu ya zamani, yaani dhambi na matendo mabaya. Lakini tule mkate usio na chachu. Huu ni mkate wenye ukweli na chachu njema.

Katika barua yangu niliwaandikia kuwa msishirikiane na wazinzi. 10 Lakini sikuwa na maana ya watu wa ulimwengu huu. La sivyo ingewalazimu kuhama katika ulimwengu huu ili mweze kujitenga na wazinzi au walio walafi na waongo, au wale wanaoabudu sanamu. 11 Nilikuwa na maana kuwa msishirikiane na mtu yeyote yule anayedai kuwa anaamini lakini anaendelea kuishi katika dhambi. Usimkaribishe nyumbani kwa chakula kaka ama dada aliye mzinzi, mlafi, anayeabudu sanamu, mtukanaji, mlevi au mwongo.[d]

12-13 Si kazi yangu kuwahukumu wasio sehemu ya kundi la waamini. Mungu atawahukumu, lakini ni lazima mwahukumu wale walio katika kundi lenu. Maandiko yanasema, “Mwondoe mwovu katika kundi lako.”(A)

Footnotes

  1. 5:5 tabia yake ya kujisifu Kwa maana ya kawaida, “Mwili wa dhambi”, ama “damu na nyama”.
  2. 5:7 mkate wa Pasaka Mkate maalum usio na chachu (chachu) ambao Wayahudi walikula katika mlo wa Pasaka. Paulo anamaanisha kuwa waamini hawana dhambi, kama ambavyo mkate wa Pasaka haukuwa na chachu.
  3. 5:7 Mwanakondoo wetu wa Pasaka Yesu alikuwa sadaka kwa ajili ya watu wake, kama mwanakondoo aliyechinjwa kwa ajili ya Sikukuu ya Pasaka ya Kiyahudi.
  4. 5:11 mwongo Kulaghai watu ili kuwaibia.