Add parallel Print Page Options

Simulizi Kuhusu Mkulima Aliyepanda Mbegu

(Mt 13:1-9; Lk 8:4-8)

Kwa mara nyingine Yesu akaanza kufundisha kando ya ziwa. Umati wa watu ukakusanyika kumzunguka, naye akapanda ndani ya mtumbwi ili akae na kufundisha huku mtumbwi ukielea. Yesu akawafundisha mambo mengi kwa simulizi zenye mafumbo. Katika mafundisho yake alisema:

“Sikilizeni! Mkulima mmoja alitoka kwenda kupanda mbegu. Alipokuwa akitupa na kuzisambaza mbegu hizo nyingine ikaanguka katika njia, na ndege wakaja na kuila. Mbegu nyingine ikaanguka juu ya uwanja wenye miamba, mahali ambapo hapakuwa na udongo wa kutosha. Hiyo mbegu ilichanua haraka kwani udongo ule haukuwa na kina cha kutosha. Lakini jua lilipochomoza, ule mmea uliungua na kwa sababu haukuwa na mizizi ya kutosha ulinyauka. Mbegu nyingine ilianguka kwenye magugu yenye miiba, na miiba ile ilikua na hatimaye kuibana sana na hivyo haikuzaa chochote. Mbegu nyingine ilianguka kwenye udongo mzuri, nayo ikaota, ikakua na kuzaa matunda; ikazaa mara thelathini, sitini na hata mia zaidi.”

Kisha akasema, “Kila mwenye masikio mazuri ayasikie haya.”

Kwa nini Yesu Alitumia Simulizi Kufundisha

(Mt 13:10-17; Lk 8:9-10)

10 Yesu alipokuwa peke yake, wale waliomzunguka na wale kumi na wawili walimuuliza kuhusu mifano hiyo.

11 Akawaambia, “Ni ninyi tu mliojaliwa kuzifahamu siri juu ya Ufalme wa Mungu. Lakini kwa wale walio nje nanyi mambo yote yatasemwa kwa simulizi zenye mafumbo, 12 Ili kwamba,

‘japo watatazama
    sana hawataona,
na kwamba japo watasikia
    sana hawataelewa;
vinginevyo,
    wangegeuka na kusamehewa!’”(A)

Read full chapter

Mfano Wa Mbegu

Wakati mwingine tena Yesu alianza kufundisha kando ya ziwa. Watu wengi walikusanyika wakasongamana mpaka ukingoni mwa ziwa. Ikambidi Yesu aingie kwenye mashua, akaketi humo. Akawafundisha mambo mengi kwa kutumia mifano na katika mafundisho yake akasema:

“Sikilizeni! Mkulima mmoja alikwenda kupanda mbegu zake. Alipokuwa akipanda, baadhi ya mbegu zilianguka njiani; ndege wakaja wakazila. Nyingine zilianguka kwenye mwamba ambapo kuli kuwa na udongo haba; zikaota haraka. Kwa kuwa udongo haukuwa na kina, jua kali lilipowaka zilinyauka na kukauka kwa kuwa hazi kuwa na mizizi. Mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, miiba hiyo ikakua ikazisonga kwahiyo hazikuzaa matunda.

Na mbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri, zikaota vizuri na kukua; zikazaa matunda; moja thelathini, nyingine sitini na nyingine mia moja.” Kisha Yesu akasema, “Mwenye nia ya kusikia na asikie.”

Kwa Nini Yesu Alitumia Mifano

10 Alipokuwa peke yake, baadhi ya wale waliokuwepo, pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili, walimwuliza kuhusu mifano yake. 11 Akawaambia, “Siri ya Ufalme wa Mungu imefunuliwa kwenu, lakini kwa wale walioko nje ya Ufalme wa Mungu, kila kitu husemwa kwa mifano 12 ili: ‘Kutazama watazame lakini wasione, kusikia wasikie lakini wasielewe. Kwa maana kama wangesikia na kuelewa wangegeuka na kutubu, wakasamehewa.’ ”

Read full chapter